Ajifungua pacha wanne Geita

Mkazi wa Mtaa wa CCM mji mdogo wa Katoro Wilaya ya Geita, Happiness Yohana (kushoto) ambaye amejifungua watoto wa nne katika kituo cha afya Katoro.

Muktasari:

Mwanamke aliyejifungua watoto wanne wilayani Geita aomba Watanzania wamsaidie ili aweze kuwalea watoto wake kutokana na hali duni kiuchumi aliyonayo.

Geita. Mkazi wa Mtaa wa CCM mji mdogo wa Katoro Wilaya ya Geita, Happiness Yohana (30) amejifungua watoto wanne katika kituo cha afya Katoro.

Mwanamke huyo aliyejifungua Desemba 7, 2022 kwa njia ya kawaida, huu ni uzao wake wa tatu na waliozaliwa wawili ni wavulana na wawili wa kike huku wawili wakiwa na kilogram 1.5 mwingine kilogram 1.4 na kilogram 1.3.

Akizungumza kituoni hapo, muuguzi aliyemzalisha Catherine Paul amesema mama huyo amejifungua salama na alifika hospitali kiwa tayari ana uchungu na aliposaidiwa watoto walitoka kwa awamu bila usumbufu.

“Alipofika alikuwa hajawahi kuja hapa kliniki lakini kadi yake inaonyesha ameenda kliniki mara moja zahanati binafsi Novemba, nilipomuona na kumpima niligundua tumbo sio la kawaida na alikua karibu mtoto atoke.

“Nilimzalisha mtoto wa kwanza lakini tumbo ilikuwa bado kubwa, ndipo nilimuita daktari akanikuta tayari nimewatoa watoto watatu na kwa neema ya Mungu tulifanikiwa kuwatoa watoto wanne.

“Haikuwa rahisi kwa sababu alikuja amekamilika hata muda wa kumpima mlalo wa mtoto haukuwepo ilikuwa kazi ngumu, uzuri Mungu alisaidia wakawa wamelala vizuri na walitoka salama na hii ilikua mara ya kwanza kuzalisha watoto wanne nimezalisha mapacha wawili mara nyingi,” amesema Catherine.

Muuguzi huyo amesema kwa hali aliyompokea nayo mama huyo inaonyesha hana uwezo wa kuwalea mwenywe kutokana na hali aliyokuja nayo ambayo hata mavazi hakuwa nayo na hali yake ya afya ni dhoofu.

Mama wa watoto hao Happines Yohana amesema mimba ya watoto hao ilikua tofauti na nyingine kutokana na kumlemea mapema akiwa na miezi mitatu.

“Mimba ilikua imenilemea hadi nikawa nashangaa nimebeba nini mana tumbo lilikuwa kubwa sana hata kutembea nilikua nashindwa,” amesema.

Mama huyo amesema licha ya kujifungua salama lakini ana hofu ya kuwalea wanae kutokana na uwezo mdogo wa kiuchumi katika familia yake na kuwaomba watanzania kumsaidia ili aweze kupata maziwa na mavazi kwa ajili ya wanae.

“Nimezaa watoto wanne uwezo sina hata ndugu zangu ni watu wa kawaida naomba msaada ili niweze kuwalea vizuri wakue,” amesema Happiness.

Kwa mujibu wa Happiness hii ni mara ya kwanza kuzaa mtoto zaidi ya mmoja lakini familia yao inawatoto mapacha kwa upande wake na hata upande wa mume.

"Kaka yangu mke wake amezaa mapacha wawili mara tatu na hata niliko olewa kuna mapacha," amesema.

Kutokana na uzito mdogo walionao watoto hao wamelazimika kupelekwa katika hospitali ya rufaa ya Geita kwa uangalizi maalum.

Mratibu wa tiba katika hospitali hiyo, Dk Pasclates Ijumba amesema watoto wako salama na wako kwenye kitengo cha watoto njiti na wataendelea na huduma hospitalini hapo hadi waongezeke uzito na watakaa kwa kipindi cha wiki tano hadi sita.

Dk Ijumba amesema tukio la mama kuzaa watoto wanne kwa wakati mmoja ni tukio la kwanza katika hospitali hiyo na mapema mwaka huu wanawake wawili kutoka Katoro walijifungua watoto watatu kwa nyakati tofauti.