Prime
Mbinu saba za kukuza uwezo wa akili, kufikiri

Muktasari:
- Pamoja na mbinu hizo kukuza uwezo wa kufikiri, pia wataalamu hao wanasema zinaimarisha afya ya mwili, kuondoa msongo wa mawazo na kukuza kumbukumbu.
Mwanza. Unajua kuwa akili yako inaweza kuimarika kwa mambo kadhaa madogomadogo unayoweza kuyafanya kila siku? Wataalam wa afya wameeleza mbinu saba za kuboresha uwezo wa akili na kufikiri.
Pamoja na mbinu hizo kukuza uwezo wa kufikiri, pia wataalamu hao wanasema zinaimarisha afya ya mwili, kuondoa msongo wa mawazo na kukuza kumbukumbu.
Wanasema kuna tabia na mazoezi yanayoweza kusaidia na kukuza uwezo wa akili, na kwamba endapo yatazingatiwa, yanaweza kupunguza kwa kiasi kikubwa uwezekano wa mtu kupata magonjwa ya akili.
Mazoezi ya mwili
Wataalamu wa afya wanasema, kufanya mazoezi ya mwili kama kutembea, kuogelea, na kuendesha baiskeli, pamoja na mazoezi ya akili kama kusoma, kujifunza lugha mpya, na tahajudi (tafakuri), ni njia madhubuti za kuongeza uwezo wa kufikiri na kumbukumbu.
Daktari katika Hospitali ya Nyanza jijini Mwanza, Dk Jafar Almasi, anasema mazoezi hayo yanaweza kukuza uwezo wa akili.
"Ili uweze kukuza uwezo wako wa akili, inashauriwa utembee au ufanye mojawapo ya mazoezi haya angalau dakika 150 kwa wiki ukigawanya ndani ya siku tano,"anasema.
Anaongeza: "Ukiweza kufanya mazoezi haya, yanarahisisha mzunguko wa damu kwenye ubongo au kwenye mwili kwa ujumla. Hii husaidia kuzuia magonjwa yanayosababishwa na matatizo ya ubongo,"
Akitolea mfano ugonjwa wa kupoteza kumbukumbu (dementia) ambao mara nyingi huathiri watu kuanzia miaka 50 na zaidi, anasema mazoezi hayo husaidia sana kupunguza hatari hiyo.
"Unaweza kutenga angalau dakika 30 kwa siku kwa ajili ya mazoezi haya au hata zaidi ya hapo,"anaeleza Dk Almasi
Tafiti zilizofanywa na profesa Wendy Suzuki katika Chuo Kikuu cha New York, zimethibitisha kuwa mazoezi ya mwili yanachochea uwezo wa ubongo kujifunza na kujiunda upya. Tafiti zake zilizochapishwa mwaka 2013 zinaonyesha faida za kutembea, kuogelea na mazoezi mengine ya mwili kwa afya ya akili.
Mazoezi ya akili
Haya ni mazoezi yanayochangamsha ubongo. Mazoezi hayo ni pamoja na kusoma vitabu, kucheza michezo ya kutumia akili kama bao na kutegua mafumbo, kujifunza lugha mpya na ujuzi mpya.
"Mfano, mimi nikiwa daktari, naweza pia kujifunza kushona. Hii husaidia kuchangamsha ubongo, kuondoa msongo wa mawazo na hivyo kukuza uwezo wa kufikiri na kupunguza uwezekano wa kupata magonjwa ya akili,"anasema Dk Almasi
Utafiti uliofanywa mwaka 2017 na Chuo kikuu cha Cambridge cha nchini Uingereza, ulionyesha kuwa kujifunza lugha mpya huchochea sehemu mbalimbali za ubongo na kuongeza uhusiano kati ya seli za neva, hivyo kuboresha uwezo wa kufikiri na kumbukumbu.
Kulala vizuri
Tabia nyingine inayosaidia ni kukuza akili au kufikiri ni kulala kwa muda mzuri na kwa ubora.
Wataalamu wanashauri mtu alale angalau saa saba hadi nane kwa siku. Wanasema si vizuri kulala muda mfupi sana wala muda mrefu sana. Kwa mfano, mtu analala saa 10 au 15, hiyo si afya.
Mbali na muda, ni muhimu mtu alale na apumzike vizuri, ili kulala vizuri, ni vyema kuwahi kulala, kulala ukiwa hauna msongo wa mawazo, na kuzingatia mazingira ya usingizi.
Utafiti uliofanywa na Shirika la Afya Duniani (WHO) kupitia mradi wa SAGE (Study on global AGEing and adult health), ulibaini kuwa watu waliolala kati ya saa sita hadi tisa walifanya vizuri zaidi katika vipimo vya uwezo wa akili kuliko wale waliolala chini ya saa sita au zaidi ya saa tisa.
Vipimo hivyo vilihusisha uwezo wa kukumbuka mambo kwa haraka, kutaja maneno kwa ufasaha pamoja na majaribio ya kumbukumbu za tarakimu.
Utafiti huo ulihusisha watu wazima wenye miaka 50 na kuendelea kutoka nchi sita za China, Ghana, India, Afrika Kusini, Mexico na Urusi.
Kwa mujibu wa matokeo ya utafiti huo uliochapishwa mwaka 2014, watu waliolala kwa muda mfupi sana au mrefu kupita kiasi, walionesha kushuka kwa viwango vya utendaji wa akili, ikilinganishwa na wale waliopata usingizi wa saa sita hadi tisa.
Tahajudi
Tahajudi ni zoezi lingine linalosaidia kupunguza mawazo. Mfano, kukaa mwenyewe mahali tulivu ukiwa umefumba macho, unavuta hewa taratibu na kuachia. Hii husaidia kupunguza msongo wa mawazo na kuongeza uwezo wa kuzingatia.
"Inashauriwa kwa siku mtu awe na muda angalau mara moja wa kufanya tafakari...kukaa sehemu tulivu, kuvuta pumzi, na kuwaza kwa utulivu kuhusu maisha yake,"anaeleza.
Uhusiano na jamii
Tabia nyingine muhimu ni kuwa na uhusiano mzuri na jamii. Usijitenge au kujifungia pekee nyumbani. Kukutana na watu husaidia kuondoa mawazo na msongo wa mawazo, hivyo kukuza ustawi wa akili.
Lishe bora
Lishe bora pia husaidia kukuza uwezo wa akili. Ni vyema kula vyakula vyenye virutubisho muhimu kama omega-3 vitamini na madini muhimu kwa afya ya ubongo.
Kuepuka vitu hatari kwa ubongo
Ni muhimu pia kupunguza matumizi ya vitu vinavyoathiri ubongo. Mfano dawa z kulevya, matumizi mabaya ya simu na mitandao ya kijamii.