Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Wajane Geita washauriwa kutorubuniwa kuingia ndoa za shinikizo

Muktasari:

  • Siku ya wajane Duniani huadhimishwa kila Juni 23 ya kila mwaka.Kwa mujibu wa Katibu wa Chama cha Wajane mkoani humo Sara Wambura, amesema wajane wengi wanapitia maisha ya mateso baada ya kufiwa, ikiwa ni pamoja na kudhulumiwa mali walizoachiwa, kushinikizwa kuolewa tena, na wengine kuachwa bila msaada wowote wa kifamilia.

Geita. Licha ya changamoto mbalimbali zinazowakabili, ikiwemo kunyanyapaliwa, kutengwa na kunyang’anywa mali, wajane mkoani Geita wameshauriwa kutokukubali kurubuniwa kuingia katika ndoa nyingine kwa shinikizo.

Badala yake, wametakiwa wajitambue, wawalee watoto wao kwa upendo, na wajielekeze katika shughuli za kujitegemea ili kujijengea maisha bora na yenye heshima.

Ushauri huo umetolewa leo Julai 3, 2025, mjini Geita wakati wa maadhimisho ya Siku ya Wajane Duniani, yaliyowaunganisha wajane kutoka maeneo mbalimbali ya mkoa huo kwa lengo la kushirikishana uzoefu na kupeana faraja.

Katibu wa Chama cha Wajane mkoani humo Sara Wambura, amesema wajane wengi wanapitia maisha ya mateso baada ya kufiwa, ikiwa ni pamoja na kudhulumiwa mali walizoachiwa, kushinikizwa kuolewa tena, na wengine kuachwa bila msaada wowote wa kifamilia.

“Mimi mwenyewe nilifiwa nikiwa na miaka 23 na watoto wadogo. Familia ya mume wangu walitaka niolewe na ndugu yake. Nilipokataa, walininyima kila kitu nimeanza maisha upya lakini kwa shida sana,” amesema Wambura.

Mjane mwingine, Mariam Absalome, aliyeachwa mjane tangu mwaka 2014, amesema kuwa jamii huwageuka wajane mara tu baada ya msiba, huku wanawake wakiwa wa kwanza kuwatenga kwa hofu kuwa watawanyang’anya waume zao.

“Ujane siyo kosa. Lakini, wanawake wanatuogopa  wanaona tutawaibia waume zao. Ndugu wa mume nao wanakutenga, unabaki na watoto tu. Ni maisha magumu sana,” amesema Mariam.

Akisoma risala kwa mgeni rasmi ambae ni Mkuu wa Mkoa wa Geita Martine Shigela, kaimu katibu wa chama hicho Christina Gamba amesema wajane wanakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo shinikizo la kuolewa kwa lazima bila kuzingatia hali ya kihisia au mazingira ya watoto.

Changamoto nyingine ni ile ya afya ya akili na msongo wa mawazo unaopelekea kuzama kwenye pombe na biashara haramu hivyo kuathiri malezi ya watoto.

Kutokujua haki zao kisheria imetajwa kuwa changamoto inayowasababisha kudhulumiwa na kunyimwa haki, huku ukosefu wa vyanzo vya mapato ikisababisha wajane wengi kuishi maisha ya kubahatisha na kutelekeza familia.


 Akizungumza katika maadhimisho hayo, Mkuu wa Mkoa wa Geita, Martin Shigella, amesema Serikali itaendelea kushirikiana na taasisi zinazowahudumia wajane ili kuhakikisha wanapata msaada wa kisheria, kiuchumi na kisaikolojia.

“Wajane wengi huanza kunyanyaswa mara tu baada ya kuondokewa na wenza wao. Chama hiki kiwe jukwaa la kusema ukweli, kusaidiana na kusaidia wale waliokataliwa, tuwaunganishe wajane waone liko tumaini na yako maisha mbele pamoja na yote yaliyotokea,”amesema Shigella.