Mara yapokea Sh10 bilioni za tozo kujenga vituo vya afya

Mkuu wa Mkoa wa Mara, Ally Hapi (wa pili kushoto) akizungumza baada ya kukagua mradi wa ujenzi wa kituo cha afya cha Rwamlimi kinachojengwa kupitia fedha za tozo. Picha na Beldina Nyakeke

Muktasari:

  • Mkuu wa Mkoa wa Mara, Ally Hapi amesema mkoa huo umepokea Sh2.5 bilioni kwaajili ya kuboresha miundombinu ya afya zilizotokana na tozo za miamala ya simu.

Musoma. Mkuu wa Mkoa wa Mara, Ally Hapi amesema mkoa huo umepokea Sh2.5 bilioni kwaajili ya kuboresha miundombinu ya afya zilizotokana na tozo za miamala ya simu.

Amesema fedha hizo zitatumika kujenga vituo 10 vya afya katika mkoa huo huku kipaumbele kikitolewa kwa tarafa ambazo hazikuwa na vituo vya afya.

Akizungumza wakati wa kukagua ujenzi wa kituo cha afya cha Rwamlimi katika Manispaa ya Musoma, Hapi amesema kuwa fedha hizo zilipokelewa mwezi Novemba mwaka jana ikiwa ni awamu ya kwanza ya utekelezaji wa miradi ya ujenzi wa vituo vya afya mkoani humo.

Amesema kuwa fedha hizo za awamu ya kwanza zitatumika kujenga majengo ya wagonjwa wa nje, maabara na sehemu ya kuchomea taka huku fedha za awamu ya pili ambazo zinatarajiwa kupokelewa kati ya mwezi Februari na Machi mwaka huu zitatumika kukamilisha vituo hivyo.

"Awamu ya pili ya fedha za tozo itatumika kujenga majengo ya mama na mtoto, wodi za kulaza wagonjwa na majengo ya upasuaji tunataka huduma zote muhimu za afya zipatikane kwenye vituo vya afya ili kupunguza misongamano kwenye hospitali za wilaya na mkoa" amesema Hapi

Akizungumzia ujenzi wa ujenzi wa kituo cha afya cha Rwamlimi, Mkuu wa Wilaya ya Musoma, Dk Halfan Haule amesema kuwa Manispaa ya Musoma imepokea Sh250 milioni kwaajili ya ujenzi wa mradi huo ambao ulianza mwezi Desemba mwaka jana.

Amesema kuwa mradi huo ukikamilia utatoa huduma kwa wakazi wa kata nne zilizo jirani na eneo hilo ambapo jumla ya watu 72,002 wakitarajiwa kunufaika.

Amezitaja kata hizo kuwa ni Rwamlimi, Mshikamano, Kwangwa na Nyakato huku akisema kuwa kukamilika kwa mradi huo kutasogeza huduma za afya karibu zaidi na wananchi.

Mkazi wa kata ya Songambele katika kata ya Rwamlimi, Sophia Majura amesema kuwa ili mradi huo uweze kuwa na manufaa kwa wakazi wa kata hizo ni lazima kuwepo na jengo la mama na mtoto pamoja na chumba cha upasuaji.