Marekani yaipa Tanzania mabilioni kukabiliana na Uviko 19

Muktasari:
- Serikali ya Marekani kupitia Shirika la Maendeleo ya Kimataifa la Marekani (USAID) imetoa dola milioni 44 kuisaidia Tanzania kukabiliana na ugonjwa wa Uviko 19.
Iringa. Serikali ya Marekani kupitia Shirika la Maendeleo ya Kimataifa la Marekani (USAID) imetoa dola milioni 44 kuisaidia Tanzania kukabiliana na ugonjwa wa Uviko 19.
Ufadhili huo kwa kiasi kikubwa umesaidia chanjo ya Uviko 19 kuwafikia watu wote kwa usalama na uhakika.
Hayo yamesemwa na mkurugenzi mkazi wa Shirika la Marekani la Maendeleo Kate Somvongsiri leo Jumamosi Agosti 20, 2020 wakati akitoa taarifa kwa wanahabari mkoani Iringa kuhusu mwitikio wa Shirika la Maendeleo ya Kimataifa katika mapambano dhidi ya Uviko 19 nchini Tanzania.
Amesema programu hiyo inalenga kupunguza vifo na kukabiliana na maambukizi ya virusi kabla ya upatikanaji wa chanjo na kutoa taarifa kuhusu athari za kiafya na kupambana na taarifa zisizo sahihi za Uviko 19.
"Chanjo ni mojawapo ya mbinu bora za kukabiliana na janga hili na kusaidia kuzuia mlipuko wa virusi vingine vitakavyotishia afya ya Watanzania na kila mtu duniani kote, Marekani inaongeza juhudi kusaidia nchi."
"Kupata, kusambaza na kusimamia chanjo kwa ufanisi katika kuunga mkono juhudi hizi USAID ilichangia dola milioni 25 kupitia ushirikiano na Tanzania chini ya mpango wa Serikali ya Marekani wa upatikanaji chanjo Duniani au Global Vax," amesema.
Mganga mkuu wa Mkoa wa Iringa, Dk Mohamed Mang'una amesema wananchi 337,047 sawa na asilimia 50.2 wamepata chanjo ya Uviko 19 katika Mkoa wa Iringa hadi Agost8 18, 2022 huku akieleza kuwa hadi kufikia desemba Mkoa utakuwa umechanja zaidi ya asilimia 70.
Kwa upande wake mkurugenzi msaidizi kitengo cha elimu ya afya kwa umma Idara ya Kinga Wizara ya Afya, Dk Anna Kasangala amesema kampeni ya bega kwa bega ujanja kuchanja imeleta mafanikio katika Mikoa mitano kupitia mziki na wasanii.
"Wananchi wameendelea kujitokeza na kuchanja mpaka sasa asilimia 54 bara na visiwani tukiweka nguvu na kuwaleta wananchi pamoja mpaka kufikia desemba nchi itakuwa imechanja na kufika asilimia 70 kama ambavyo Marekani inawataka," amesema.
Amesema ugonjwa wa Uviko 19 bado upo nchini na wagonjwa wapo lakini hakuna vifo vitokanavyo na ugonjwa hup na ndio sababu wanahimiza watu kuchanja.