Marekani yasitisha mazungumzo na Taliban

Rais wa Marekeni, Donald Trump

Muktasari:

Raia wa Afghanistan wanajiandaa kwa uwezekano wa mashambulizi mapya ya kundi la Taliban baada ya kukwama kwa mazungumzo na Marekani

Afghanistan. Rais wa Marekeni, Donald Trump amefuta ghafla  mazungumzo na kundi la Taliban ambalo limeapa kuendeleza vita dhidi ya kile linachokiita ukaliaji wa kigeni.

Wachambuzi wa masuala ya siasa wanasema kuwa maamuzi hayo ya Marekani yanaweza kusababisha ghasia baina ya raia wa Afghanistan na kundi hilo la Taliban.

Uamuzi wa Rais Trump ulitolewa na Ikulu ya Marekani mwisho ni wiki kupitia tangazo lake ambali lilitolewa muda mfupi kabla ya msururu wa siku muhimu nchini Afghanistan ikiwa ni pamoja na maadhimisho ya kifo cha kamanda aliyekuwa mpinzani mkubwa wa kundi la Taliban, Ahmad Shah Massoud

Kundi hilo la Taliban lilishambulia takribani wilaya mbili katika eneo la Kaskazini Mashariki la Mkoa wa Takhar usiku kucha lakini hakukuwa na ripoti juu ya majeruhi ama waathiriwa iliyotolewa.

Kundi hilo limeshambulia miji mikuu ya mikoa mitatu mapema mwezi huu wakati lilipokuwa likikamilisha makubaliano na Marekani juu ya kusitisha vita ambavyo vimedumu kwa takriban miaka 18.

Jumapili iliyopita msemaji wa Rais wa Afghanistan, Sediq Seddiqqi aliwaambia wanahabari mjini Kabul kwamba haina maana kuendeleza mazungumzo hayo ambayo hayatakuwa na mwisho mwema kuhusiana na ghasia zinazotekelezwa na kundi hilo la Taliban. 

Hata hivyo, waziri wa Mambo ya ndani wa Marekani, Mike Pompeo alisema kuwa Wataliban walivuka mipaka kwa kutekeleza shambulizi  la bomu lililotegwa ndani ya gari katika eneo la kidiplomasia karibu na ubalozi wa Marekani mjini Kabul na kumuua mwanajeshi wa Marekani na hilo ndilo lililosababisha Rais Trump kujiondoa katika mazungumzo hayo ya mkataba wa amani wa Afghanistan na Camp David.

Pompeo alisema sasa itabidi kundi hilo la wataliban kubadilisha mienendo yake ingawa hakusema iwapo mazungumzo hayo ya amani yatarejelewa na ni lini yatarejelewa.