Masauni avunja ukimya taasisi za dini kusaidia vikundi vya kigaidi

Waziri wa Mambo ya Ndani, Hamad Masauni, akizungumza wakat wa uzinduzi wa kampeni ya usajili wa jumuiya za kiraia iliyokuwa na kauli mbiu ya 'Usajili wa jumuiya kwa maendeleo na ustawi wa Taifa letu'.

Muktasari:

 Wadau wa jumuiya za kiraia wajengewa uwezo kuhusu umuhimu wa kuzisajili taasisi hizo,  huku Serikali ikisema kwa siku za hivi karibuni  baadhi ya jumuiya hizo zinafanya mambo yanayohatarisha amani na kuvisaidia vikundi vya kigaidi.

Dar es Salam.Waziri wa Mambo ya Ndani, Hamad Masauni amesema licha ya jumuiya za kiraia kuwa na mchango katika kuleta mabadiliko chanya katika jamii, baadhi zina changamoto ikiwemo kujihusisha na vitendo vinavyohatarisha amani na usalama wa Taifa.

Waziri Masauni ametoa kauli leo Jumanne Machi 26, 2024 wakati akizindua kampeni ya usajili wa jumuiya za kiraia iliyokuwa na kauli mbiu ya 'Usajili wa jumuiya kwa maendeleo na ustawi wa Taifa letu'.

Kampeni hiyo inakwenda sambamba na kuwajengea uelewa viongozi wa jumuiya kuhusu usajili na usimamizi wa jumuiya hizo za kidini, kijamii,kitaaluma na kiuchumi.

Miongoni mwa waliohudhuria ni pamoja maofisa watendaji kata na makatibu tawala ambao jumuiya hizo zipo katika maeneo yao.

Amesema hivi karibuni kumeibuka wimbi la baadhi ya jumuiya kutumika katika kusaidia makundi yenye dhima ya kigaidi, kusambaza propaganda za uchochezi, kuwasilisha ajenda za kigeni zinazohatarisha maslahi ya Taifa ikiwemo mmomonyoko wa maadili.

"Kuna muhimu kwa jumuiya za kiraia kufanya kazi kwa kuzingatia kanuni za maadili, uwazi, na uwajibikaji ili kuhakikisha wanachangia katika maendeleo ya jamii bila kuhatarisha ulinzi na usalama wa nchi..

"Serikali pia ina jukumu la kusimamia na kudhibiti shughuli za jumuiya za kiraia ili kuhakikisha zinafanya kazi kwa kuzingatia sheria na taratibu za nchi.

Mbali na hilo, Masauni amesema imebainika uwepo kwa changamoto ya uanzishwaji holela na utitiri wa nyumba za ibada katika maeneo mbalimbali hapa nchini.

Ameongeza kuwa baadhi taasisi za kidini ikiwemo  makanisa na misikiti zimebainika kujengwa katikati ya makazi ya watu na kusababisha mrundikano wa taasisi nyingi kwenye eneo dogo.

Waziri Masauni amesema  baadhi ya taasisi hizo zimekuwa zikitumia sauti za juu inayosababisha adha na usumbufu katika jamii.

Pia amesema baadhi ya jumuiya za kiraia zimeripotiwa kujihusisha au kutumika katika kufanikisha kutendeka kwa makosa ya jinai na vitendo vingine vyenye madhara kwa jamii.

"Miongoni mwa makosa hayo ni utakatishaji wa fedha haramu, ugaidi na ufadhili wa shughuli za kigaidi, usafirishaji haramu wa binadamu, biashara haramu ya silaha na uwepo wa jumuiya za kidini zinazotoa mafundisho potofu na hatarishi kwa usalama wa raia," amesema.

Kwa mujibu wa Masauni, changamoto hizo zinahitaji ushirikiano wa pamoja katika kuzitatua, ili kuendelea kudumisha hali ya utulivu na usalama katika maeneo mbalimbali.


Faida za jumuiya za kiraia

Hata hivyo, Masauni amesema jumuiya za kiraia zina mchango mkubwa katika kuleta mabadiliko chanya katika jamii na kuchangia katika maendeleo endelevu ya jamii na Taifa.

Pia, Waziri Masauni amesema jumuiya hizo zina mchango katika kuchochea ubunifu na ukuaji wa uchumi, utoaji wa huduma za kijamii kama vile shule na hospitali.

"Usajili unaweza kusaidia kulinda haki na maslahi ya jumuiya za kiraia na wanachama wanapata ulinzi dhidi ya unyanyasaji, ukandamizaji au  ukiukwaji wa haki zao na ulinzi dhidi ya vitendo vya ubadhirifu na ufujaji wa fedha na mali za jumuiya zao," amesema Waziri Masauni.

Msajili wa jumuiya za kiraia, Emmanuel Kihampa amesema taasisi hiyo ilianza kutekeleza majukumu yake tangu mwaka 1955 hadi Januari mwaka huu, kuna jumuiya za kiraia zaidi ya 10,000, hata hivyo kutokana na ukongwe huo zipo baadhi hazifanyi kazi.

"Ndio maana Serikali imekuwa ikifanya ukaguzi na uhaulishaji wa vyeti  kwa lengo kutambua jumuiya zilizoko hai na zisizotekeleza majukumu yake, mchakato uliokamilika Mei 2023.

"Sasa hivi tunaendelea na mchakato wa kubaini taasisi ambazo haziko hai tunaziondoa katika usajili ndio maana kuanzia Januari mwaka huu tumetoa orodha ya taasisi zaidi ya 1,000 zile ambazo zitashindwa kuthibitisha uhai wake ndani ya siku 90 tutazifuta " amesema Kihampa.