Masele ajitosa kumrithi Ndugai

Stephen Masele akizungumza baada ya kuchukua fomu.

Muktasari:

Aliyewahi kuwa Makamu wa kwanza wa Rais katika Bunge la Afrika (PAP), Stephen Masele amechukua fomu ya kuomba kuteuliwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM) kugombea nafasi ya Spika wa Bunge la Tanzania.

Dar es Salaam. Aliyewahi kuwa Makamu wa kwanza wa Rais katika Bunge la Afrika (PAP), Stephen Masele amechukua fomu ya kuomba kuteuliwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM) kugombea nafasi ya Spika wa Bunge la Tanzania.

Masele ambaye ni mbunge wa zamani wa Shinyanga Mjini amefika leo saa 4:30 asubuhi ofisi za Makao Makuu ya Chama cha Mapinduzi (CCM) kuchukua fomu hiyo.

Patrick Nkamah ni kada wa kwanza kuchukua fomu hiyo saa 8:26 asubuhi ambaye haikuwa rahisi kumpata kwa simu yake ya mkono.

Hatua hiyo inajitokeza baada ya uongozi wa CCM jana kutangaza rasmi ratiba ya uchukuaji fomu hizo ili kupata mwakilishi wa chama hicho atakayegombea nafasi iliyoachwa wazi na Job Ndugai baada ya kujiuzulu siku chache zilizopita.

Akizungumza na Mwananchi, Masele amesema amechukua fomu baada ya kujipima sifa za kugombea nafasi hiyo.

“Kwanza ni matakwa ya kikatiba, Katiba yetu inatoa nafasi kwa mtanzania yeyote mwenye sifa za kugombea ubunge anaweza kugombea nafasi ya Spika wa bunge hilo,” amesema Masele.

“Kwa hiyo nafasi yangu kama Mtanzania na mwanachama wa CCM nimeamua niombe ridhaa kwa chama changu kinifikirie katika nafasi hiyo.”

Katika ufafanuzi wake, Masele amesema endapo atapewa nafasi hiyo atatoa mchango wake katika ufanikishaji wa shughuli za Bunge kwa kuzingatia Katiba ya Nchi, Kanuni za Bunge na desturi.

“Uwezo ninao, uzoefu ninao hivyo nina Imani kwamba nikifanikiwa kuwa spika nitaweza kusimamia shughuli za serikali na kuhakikisha Taifa letu linapiga hatua kimaendeleo, kwa ufupi mniombee (Watanzania).”

Kada wa tatu aliyejitokeza kuchukua fomu hiyo ni Hamidu Chamani aliyefika ofisi hizo saa 6:56 mchana.

Chamani ambaye ni kada wa miaka 17 ndani ya chama hicho amesema sababu za kugombea zinampatia uhalali huo na anaamini anaweza kuongoza bunge hilo ili kusaidia shughuli za Maendeleo kwa watanzania.

Chamani amedai kulelewa kiuongozi ndani ya umoja wa vijana wa chama hicho, akitumikia nafasi ya Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Wilaya ya Kyerwa, Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa Vijana na Mjumbe wa Mkutano mkuu wa CCM.

“Lakini niligombea ubunge Jimbo la Kyerwa Uchaguzi Mkuu wa 2020 kwa hiyo uzoefu ninao,”amesema.