Mashine za kukaushia kucha zaongezewa kodi
Muktasari:
- Serikali inapendekeza kutoza ushuru wa bidhaa kwa bidhaa za urembo, maua bandia na magari yaliyotumika.
Dodoma. Serikali imependekeza kutoza ushuru wa bidhaa kwa mashine za kukaushia rangi za kucha zinazoingizwa nchini, bidhaa za urembo, maua bandia na magari yaliyotumika.
Mbali na hizo, bidhaa nyingine zinazopendekezwa kuongezewa ushuru ni viatu vya plastiki.
Waziri wa Fedha, Balozi Khamis Mussa Omar, amesema hayo leo Juni 11, 2026 wakati akiwasilisha hotuba ya mapendekezo ya Serikali kuhusu makadirio ya mapato na matumizi kwa mwaka wa fedha 2026/27.
Amesema ushuru wa asilimia 10 kwa mashine za kukaushia rangi za kucha umeanzishwa kutokana na uwepo wa athari za kiafya zinazoweza kujitokeza kwa watumiaji wa bidhaa hizo, ikiwamo saratani.
“Hatua hii inatarajiwa kuongeza mapato ya Serikali kwa kiasi cha Sh566.5 milioni,” amesema.
Vilevile, Serikali imependekeza kuongeza ushuru wa bidhaa kutoka asilimia 10 hadi asilimia 15 kwa bidhaa za urembo zinazoingizwa nchini.
Balozi Omar amesema lengo la ongezeko hilo ni kuongeza mapato ya Serikali na kuoanisha viwango vya ushuru vinavyotozwa nchini na vile vinavyotumika katika baadhi ya nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).
Amesema Kenya, Uganda na Rwanda tayari zinatoza viwango vinavyokaribiana na hivyo, jambo linaloifanya Tanzania kuchukua hatua hiyo ili kuimarisha ushindani na usawa wa kikodi ndani ya ukanda huo.
“Hatua hii inatarajiwa kuongeza mapato ya Serikali kwa kiasi cha Sh1.91 bilioni,” amesema.
Mbali na bidhaa hizo, amesema nyingine ni viatu vya plastiki vinavyoingizwa nchini vinavyotambulika kwa HS Code 6402.99.00.
“Lengo la hatua hii ni kulinda viwanda vya ndani vinavyozalisha viatu vya plastiki na kuchochea uwekezaji ndani ya nchi. Hatua hii inatarajiwa kuongeza mapato ya Serikali kwa kiasi cha Sh10.58 bilioni,” amesema.
Waziri Omar amesema Serikali inapendekeza kuongeza ushuru wa bidhaa kwenye magari yaliyotumika yanayoingizwa nchini kutoka asilimia 15 hadi asilimia 20.
Amesema pendekezo hilo linahusu magari yenye umri wa miaka minane lakini yasiyozidi miaka 10, na kutoka asilimia 30 hadi asilimia 40 kwa magari yenye umri wa zaidi ya miaka 10 lakini yasiyozidi miaka 20.
Kwa magari yenye umri unaozidi miaka 20 na kuendelea, amesema yatatozwa ushuru wa bidhaa kwa kiwango cha asilimia 50.
“Lengo la hatua hii ni kuongeza mapato ya Serikali pamoja na kupunguza uingizaji wa magari husika ambayo kwa kiasi kikubwa yanasababisha uchafuzi wa mazingira kutokana na uwepo wa taka ngumu zinazohitaji gharama kubwa kuziteketeza. Hatua hii inatarajiwa kuongeza mapato ya Serikali kwa kiasi cha Sh106.70 bilioni,” amesema.