Mashirika yasio ya kiserikali Tanga yatakiwa kuboresha miradi

Mkuu wa wilaya ya Tanga, Dadi Kolimba akizungumza wakati wa uzinduzi wa miradi saba ya maendeleo itakayosimamiwa na Shirika lisilo la kiserikali la Tanga Yetu leo Jumanne Julai Mosi,2025.Picha na Rajabu Athumani.
Muktasari:
- Miradi ya Sh2.4 bilioni imezinduliwa jijini Tanga ambayo itahusika na masuala ya afya, michezo ,ujasiriamali, ushirikishwaji vijana, malezi na makuzi kwenye jamii.
Tanga. Mkuu wa Wilaya ya Tanga, Dadi Kolimba, ameyataka mashirika yasio ya kiserikali wilayani humo kuhakikisha miradi yote ambayo wanaianzisha inaleta manufaa kwenye jamii na kuwa endelevu.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa miradi saba ya maendeleo itakayosimamiwa na Shirika lisilo la kiserikali la Tanga Yetu leo Jumanne Julai Mosi, 2025 jijini Tanga, Kolimba amesema miradi inayokwenda kufanyika kwenye jamii inatakiwa kuwa endelevu na yenye tija.
Amesema mashirika yanatakiwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu za nchi kwa kuwa makini na kutambua wanakwenda kufanya nini na miradi husika itakwenda kunufaisha vipi jamii za rika zote, badala ya kukaa muda mfupi kuliko malengo yaliowekwa.
Kolimba amesema kwenye upande wa makuzi katika jamii vijana wapewe kipaumbele na elimu ya kuweza kujifunza jinsi ya kukabiliana na changamoto tofauti hasa za kujitafutia ajira binafsi.
Mwenyekiti wa Kamati ya Uwezeshaji wa Mradi wa Tanga Yetu, Juma Rashid amesema miradi hiyo inalenga kuleta tija katika makundi mbalimbali ya jamii ndani ya mkoa wa Tanga, kwa kuboresha huduma za kijamii, kukuza uchumi wa wananchi na kuimarisha ushiriki wao kwenye maendeleo yao.
Amesema wamezindua miradi saba yenye thamani ya Sh2.4 bilioni ambayo inahusika na masuala ya afya, michezo, ujasiriamali, ushirikishwaji vijana, malezi na makuzi kwenye jamii na yote itafanyika kwa wakati mmoja.
Mmoja wa vijana aliyeshiriki uzinduzi huo, Suzan Maingu amesema kupitia miradi hiyo wanategemea kuwezeshwa na kufikia ndoto zao hasa kwenye kipindi hiki ambacho kuna changamoto ya kukosekana ajira nchini.
Mashirika ambayo yatashirikiana kufanikisha miradi hiyo kwa jiji la Tanga ni Tanga Yetu, Botnar Foundation, Innovex na halmashauri ya jiji la Tanga kwa upande wa Serikali.