Masikio kwa Dk Mwinyi akitangaza mawaziri

Masikio kwa Dk Mwinyi akitangaza mawaziri

Muktasari:

Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi leo anatarajiwa kutangaza baraza lake la mawaziri huku masikio yakisubiri kuona jinsi atakavyoamua kuhusu Serikali ya Umoja ya Kitaifa (SUK) aliyoiahidi.

Dar es Salaam. Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi leo anatarajiwa kutangaza baraza lake la mawaziri huku masikio yakisubiri kuona jinsi atakavyoamua kuhusu Serikali ya Umoja ya Kitaifa (SUK) aliyoiahidi.

Baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 27 na 28 uliompa Dk Mwinyi ushindi wa kura 380,402 sawa na asilimia 76.27, mara kadhaa amezungumzia kuunda Serikali ya umoja wa kitaifa ili kuleta mshikamano Zanzibar.

Mshindi wa pili katika uchaguzi huo, alikuwa mgombea wa ACT-Wazalendo, Maalim Seif Sharif Hamad aliyepata kura 99,103 sawa na asilimia 19.87.

Dk Mwinyi amekwishamteua Makamu wa pili wa Rais, Hemed Suleiman Abdulla na anatazamiwa kuteua makamu wa pili wa Rais, muda wowote baada ya mazungumzo na chama kilichoshika nafasi ya pili katika uchaguzi, ambacho ni ACT Wazalendo.

Vilevile kwa mujibu wa Katiba ya Zanzibar, upo uwezekano wa Dk Mwinyi kuteua baadhi ya mawaziri kutoka katika chama hicho au kingine chochote cha siasa.

Hata hivyo, Katiba ya Zanzibar Ibara ya 39A(1) inasema endapo ndani ya siku saba baada ya Rais kushika madaraka, chama kinachostahiki kutoa makamu wa kwanza wa Rais, kitashindwa kuwasilisha jina la uteuzi, Rais, ataacha wazi nafasi hiyo na kuteua makamo wa pili wa Rais na ... atateua mawaziri na kuacha wazi nafasi za uteuzi wa chama au vyamavya upinzani.

Taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi wa Idara ya Mawasiliano na Habari Ikulu Zanzibar, Hassan Khatib Hassan, ilieleza kuwa Dk Mwinyi atatangaza baraza hilo leo kuanzia saa nne asubuhi, shughuli itakayorushwa moja kwa moja na vituo mbalimbali vya habari.

Mbali na Makamu wa pili, Abdulla Mwinyi pia alikwishamteua Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar Dk Mwinyi Talib Haji na baadaye Nahaat Mohammed Mahfoudh kuwa Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Bandari Zanzibar na Suleiman Ahmed Saleh kuwa katibu wa rais.

Dk Mwinyi amechukua nafasi ya Dk Ali Mohammed Shein aliyemaliza muda wake, ambaye wakati anaingia madarakani mwaka 2010 baraza lake lilikuwa na wizara 16.

Katika muhula wa kwanza Dk Shein aliongoza Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK) akishirikiana na Maalim Seif ambaye alikuwa makamu wa kwanza wa Rais na balozi Ally Iddi aliyekuwa makamu wa pili huku mawaziri na manaibu walitoka vyama vya CCM na CUF kwa wakati huo.

Baada ya kushinda uchaguzi mkuu uliofanyika Machi mwaka huo uliosusiwa na CUF, Dk Shein aliteua mawaziri 13 na manaibu saba, wakiwamo baadhi ya wapinzani, Hamad Rashid Mohamed na Said Soud Said ambao aliwateua kuwa wajumbe wa Baraza la Wawakilishi kisha kuwa mawaziri wakitoka vyama vya ADC na AFP.

Awatengua vigogo afya

Wakati huohuo, Dk Mwinyi jana alitengua uteuzi wa Mkurugenzi mkuu wa Afya katika wizara ya Afya, Dk Jamala Adam na Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Mnazi mmoja Dk Ali Salum Ali baada ya kutembelea hospitali ya Mnazi Mmoja na kuona changamoto katika utoaji huduma.

Taarifa ya ikulu ilieleza kuwa madaktari hao watapangiwa kazi nyingine.

Katika ziara hiyo Dk Mwinyi alitoa miezi mitatu kwa uongozi wa Wizara ya Afya kurekebisha kasoro za kiutendaji zinazosababisha kutokuwepo ufanisi katika utoaji wa huduma bora kwa wagonjwa.

Mwinyi alifanya ziara ya kushtukiza katika hospitali hiyo kwa lengo la kuangalia utoaji wa huduma kwa wagonjwa kwenye maeneo na vitengo tofauti vya hospitali hiyo kama OPD, MRI, jengo la kuhifadhia dawa na kitengo cha macho.