Maswali kura jimbo la Konde

Wanananchi wakiwa kwenye foleni ya kupiga kura katika uchaguzi wa marudio Jimbo la Konde. Picha na Jesse Mikofu

Muktasari:

  • Ni maswali katika Jimbo la Konde ambalo ndani ya kipindi kisichozidi mwaka mmoja, wananchi wake wamefanya uchaguzi wa ubunge mara tatu, huku wakishuhudia wagombea watatu wakishinda na wawili kupishana kwa idadi ya kura ndani ya miezi miwili.


Pemba. Ni maswali katika Jimbo la Konde ambalo ndani ya kipindi kisichozidi mwaka mmoja, wananchi wake wamefanya uchaguzi wa ubunge mara tatu, huku wakishuhudia wagombea watatu wakishinda na wawili kupishana kwa idadi ya kura ndani ya miezi miwili.

Katika Uchaguzi Mkuu uliofanyika Oktoba 2020, Khatibu Said Haji wa ACT-Wazalendo aliibuka mshindi kwa kupata kura 1,552 akiwashinda wagombea wa CCM, Sheha Mpemba Faki aliyepata kura 1,245, Masoud Othman Bakari (Ada-Tadea) aliyepata kura 18, Bakar Makame Khamis (ADC) aliyepata kura 38, Mohamed Suleima Said (Chadema) aliyepata kura 781, Omar Hamad Khamis (CUF) aliyepata kura 92, Abrahman Mbarouk Juma (Demokrasia Makini) aliyepata kura 26 na Abdirahim Ali Slum (NCCR-Mageuzi) kura 59.

Hata hivyo, Khatib alifariki dunia Mei 2021 katika hospitali ya Taifa Muhimbili na jimbo hilo kubaki wazi kabla uchaguzi mdogo kufanyika Julai 18, mwaka huu na Sheha Faki Mpemba (CCM), kutangazwa kuwa mshindi, lakini akajiuzulu kabla ya kuapishwa kwa madai ya familia yake kutishiwa maish

Matokeo ya uchaguzi huo yalidaiwa kutikisa siasa za Zanzibar, hasa baada ya ACT-Wazalendo kudai kuwa mgombea wao, Mohamed Said Issa ndiye aliyeshinda.

Baada ya kujiuzulu kwa Faki, Makamu wa Kwanza wa Rais, Othman Masoud alisema kada huyo kajiuzulu baada ya yeye (Othman) na viongozi wengine wa ACT- Wazalendo kuzungumza na Rais Samia Suluhu Hassan na Dk Hussein Mwinyi kuhusu dhulma iliyofanyika kwenye uchaguzi huo.

Katika uchaguzi huo, Mpemba alishinda kwa kupata kura 1,796 dhidi ya Mohamed Said Issa aliyepata kura 1,373 kati ya kura 5,050 zilizopigwa.


Meza yapinduliwa

Baada ya Mpemba kujiuzulu, uchaguzi wa marudio ulifanyika Oktoba 9 na kada wa ACT Wazalendo, Mohamed Said Issa alitangazwa mshindi kwa kura 2,391 akifuatiwa kwa mbali na Mbarouk Amour Habib wa CCM aliyepata kura 794 kati ya kura 3,408 zilizopigwa zikiwamo halali 3,338 na 70 zilzoharibika.

Msimamizi wa uchaguzi Jimbo la Konde, Abdalla Said Hemed alisema wengine walioshiriki uchaguzi huo ni Salama Khamis Omar wa CUF kura 98 na Hamad Hamis Mbarouk wa AAFP kura 55.

Wakizungumza na gazeti hili kwa nyakati tofauti, viongozi wa Chama cha Mapinduzi (CCM) na ACT Wazalendo walikuwa na mtazamo tofauti kuhusu uchaguzi na ushindi huo wa Issa.

Kaimu Naibu Mwenyekiti wa ACT- Wazalendo, Salim Bimani alisema katika uchaguzi wenye haki ni lazima wangeshinda jimbo hilo kwa kuwa hakuna rekodi ya CCM kuibuka kidedea Pemba.

Katibu Mkuu wa ACT Wazalendo, Ado Shaibu alisema changamoto zilizojitokeza Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020 zimepungua.

“Kama mnavyokumbuka, wakati ule mtu yoyote mwenye nia ovu angeweza kuandika barua kwamba mgombea fulani anajiuzulu kugombea na taarifa hizo za uongo zikafanyiwa kazi, lakini sasa huwezi kujitoa katika hatua hii,” alisema.

Akizungumzia uchaguzi huo, Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Dk Abdallah Juma Sadalla maarufu kwa jina la Mabodi, alisema hawajui kwa nini walishindwa japokuwa walijizatiti kushinda.

“Inabidi tukae kitako tujue wapi tumekosea na wapi tumefanya vizuri ili mwaka 2025 tuwe vizuri zaidi,” alisema Dk Mabodi.

Hata hivyo, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Kaskazini Pemba, Mberwa Hamad Mberwa alisema wamekubali wameshindwa kihalali, huku akisema wanachama walikuwa kwenye shughuli mbalimbali hivyo walishindwa kujitokeza kwa wingi siku ya kupiga kura.

“Maana walipomaliza uchaguzi ule wa awali wakatawanyika kwa hiyo ilikuwa ni tabu kuacha shughuli zao wakarudi tena ndani ya kipindi kifupi. Hiki ni kipindi cha karafuu hivyo watu wengi walikuwa kwenye shughuli zao,” alisema.


Maoni ya wachambuzi

Mchambuzi wa masuala ya siasa, Buberwa Kaiza alisema kilichobadilisha matokeo katika jimbo la Konde ni usimamizi uliofuata taratibu zilizopo.

Alisema wananchi waliweka msukumo kurudiwa kwa uchaguzi mpaka Fakhi akajiuzulu na Dk Mwinyi sio muumini wa siasa chafu, huenda naye alishinikiza urudiwe.

Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom), Dk Paul Loisulie alisema kura za CCM zimeporomoka, kutokana na mambo tofauti ikiwamo kukiukwa kwa baadhi ya taratibu za uchaguzi.

Naye Said Abdalla Said alisema uchaguzi huo ni aibu kwa wale wanaolaumiwa kwa muda mrefu kuwa wamekuwa wakiendesha siasa za hila na wizi wa kura. Alisema Serikali ya Umoja wa Kitaifa kwa sasa ndio inashikilia siasa za Zanzibar na kuleta umoja wa kitaifa.

“Kama unakumbuka kauli ya Othman, alisema mambo haya hayavumiliki ikizingatiwa kulikuwa na ahadi ya kufanyika uadilifu,” alisema.

Naye Saada Ali Juma alisema: “Hakuna jipya katika hilo, baada ya mbunge yule kujiuzulu na uchaguzi kurudiwa wote tulijua ACT watashinda. Sema kilichofanyika CCM ambayo ndio yenye dola hawakutaka kutoa kiti hicho kama zawadi.”


Wananchi wanena

Mwajuma Sued Ali alisema inashangaza CCM wanaposhinda, kura zinadaiwa kuibwa lakini vinaposhinda vyama vingine basi uchaguzi unatajwa kuwa huru na haki huku akihoji kwa nini kuna kasumba hiyo.

Kauli hiyo iliungwa mkono na Juma Rashid Juma akisema: “Inatakiwa ACT wawe wavumilivu wasione wao ndio wanaonewa, kama CCM wangelalamika wameibiwa unadhani tutakwenda wapi?” alihoji.

Seif Mbarouk alisema kwa uhalisia Pemba na Zanzibar kwa ujumla ni visiwa vidogo, hivyo watu wanafahamiana na vyama vya siasa vinajua kabisa ni kwa kiasi gani vinakubalika kwa wananchi.

“Hivi nani asiyejua kuwa Pemba CCM haikubaliki na haina watu? Kulazimisha ushindi ni kutafuta vurugu tu,” aliongeza.

Naye Najma Abdalla alisema wananchi hawana shida isipokuwa wanajengewa misimamo isiyo na maana na viongozi wao mara nyingi wanasikiliza yanayosemwa na viongozi.


Mbunge mteule

Naye mbunge mteule, Issa alisema siku zote uamuzi wa wananchi ungekuwa unaheshimiwa hata maendeleo ya Zanzibar yangekuwa makubwa.

“Naamini uchaguzi wa Julai 28 nilishinda lakini nikadhulumiwa, haki huwa haipotei bali hucheleweshwa. Juzi nilipewa fomu zote za matokeo katika vituo 16 vilivyotumika kupigia kura tofauti na uchagzui wa mwanzo,” alisema

“Huu ndio usawa, ninachowaahidi wananchi wa Konde ni kuchapa kazi, tushirikiane kuleta maendeleo ya jimbo letu na Zanzibar bila kujali itikadi zetu,” alisema


Hali ilivyokuwa

Uchaguzi wa safari hii haukuwa na pilikapilika za kiusalama hasa katika maeneo karibu na vituo vya kupiga kura kama ilivyozoeleka katika chaguzi nyingi.

Mbali na uchache wana usalama, hata wale waliokuwa katika vituo vya kupigia kura walionekana kusimamia vilivyo shughuli hiyo ya wananchi kutekeleza wajibu wao wa kikatiba.