Matapeli wa mitandaoni sasa kukiona

Msemaji wa Jeshi la Polisi nchini, SACP David Misime akizungumza na waandishi wa habari.

Muktasari:

  • Jeshi la Polisi nchini limeanika mbinu zinazotumiwa na matapeli kwenye mitandao kuwaibia watu huku ikisema inawafuatilia wahalifu hao ili kuwashughulikia vilivyo.

Dar es Salaam. Jeshi la Polisi nchini limetoa tahadhari kwa wananchi kuwa makini na watu au vikundi vinavyojihusisha na utapeli kwa kupiga simu au kutuma ujumbe mfupi wakiwa na lengo la kuwaibia fedha.

Kupitia taarifa iliyotolewa leo Agosti 29, 2023 na Msemaji wa Jeshi la Polisi, SACP David Misime, jeshi hilo limesema watu hao pindi wanapopiga simu hujifanya maofisa wa Serikali wenye lengo la kuwapatia watu kazi.

“Katika siku za karibuni kumeibuka tena tabia ya baadhi ya watu au vikundi vya watu kuwatapeli wananchi kwa kuwapigia simu au kuwatumia ujumbe wa maneno, huku wakijitambulisha kwa majina ya viongozi wa wizara au taasisi na kwamba wana kampeni au wanachangisha fedha kwa ajili ya kitu fulani,” imeeleza taarifa.

Imesema pia, watu hao wamekuwa wakitumia mbinu nyingine ya kupiga simu na kujitambusha kama wafanyakazi wa Ikulu au Wizarani na kuwaambia wanahitajika Dodoma kwa ajili ya kuonana na viongozi kwani wameonekana kuwa na sifa za kupewa kazi au cheo.

Taarifa imesema baada ya hapo watu hao huenda mbali zaidi na kumtaka wanayempigia simu atume fedha ili wamkatie tiketi ya ndege kwani nafasi ni chache ili aweze kuwahi na fedha yake atarejeshewa mara baada ya kuwasili Dodoma.

Jeshi limekumbusha kuwa wananchi watambue kuwa huo ni utapeli na baadhi ya watu wameshatapeliwa fedha zao kwa njia hiyo.

kadhalika limesema linaendelea kufanya uchunguzi ili kuendelea kuwabaini na kuwakamata watu hao wanaojihusisha na vitendo hivyo vya kihalifu ili kuwachukulia hatua za kisheria.

Aidha Jeshi linatoa wito kwa wananchi kuendelea kushirikiana na Polisi kwa kutoa taarifa za wahalifu na uhalifu ikiwemo uhalifu kwa njia ya mitandao mara tu wanapoona viashiria ili hatua za haraka ziweze kuchukuliwa dhidi yao.

“Mwananchi yeyote akipigiwa simu au kutumiwa ujumbe wa maneno na watu wa aina hiyo atoe taarifa katika kituo cha Polisi kilicho karibu au atume namba hiyo ya utapeli kwenda namba 15040,” imetahadharisha taarifa hiyo.