Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Matibabu bure ya fistula yawanufaisha wanawake 195 mkoani Lindi

Daktari bingwa wa magonjwa ya wanawake na upasuaji wa fistula kutoka Hospitali ya CCBRT, Dk Peter Majinge akimweleza jambo mgonjwa katika kambi ya matibabu ya bure ya fistula inayoendelea katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Lindi Sokoine. Kulia ni daktari bingwa wa magonjwa ya wanawake katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Sokoine, Jamila Athuman.

Muktasari:

  • Kambi za matibabu na mafunzo ya ujasiriamali zimeendeshwa kwa wanawake waliopona, huku wanawake 21 wakifaidika na mafunzo hayo.

Lindi. Wanawake 195 waliokuwa wakisumbuliwa na ugonjwa wa fistula ya uzazi na magonjwa mengine ya wanawake mkoani Lindi, wamepatiwa matibabu bila malipo, tangu ulipoanzishwa ushirikiano kati ya Hospitali ya CCBRT, Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Lindi-Sokoine na Shirika la Equinor Tanzania mwaka 2019.

Tangu kuanzishwa kwa ubia huo, wamekuwa wakiendesha kambi za matibabu ya bure ya fistula mkoani Lindi pamoja na kutoa mafunzo ya ujasiriamali kwa wanawake wanaotibiwa na kupona ugonjwa huo.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Jumatano Septemba 11, 2024 katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Lindi, meneja wa miradi wa Hospitali ya CCBRT, Yohana Kasawala amesema kwa mwaka huu kambi ya matibabu imeanza Septemba 9 hospitalini hapo na inatarajiwa kumalizika Septemba 13, 2024.

Amesema mpaka sasa wanawake 10 wenye ugonjwa huo wameshapatiwa matibabu.

 “CCBRT inawashukuru wadau wake wote, ikiwemo Equinor Tanzania na Serikali kwa kuendelea kutushika mkono, hivyo kuwezesha kuwafikia Watanzania wenzetu wenye mahitaji makubwa ya kiafya," amesema Kasawala.

Aidha, amemshukuru Dk Naomi Makota, msimamizi wa miradi ya jamii kutoka Equinor kwa kushiriki katika kambi hiyo inayoendelea mjini Lindi.

Kasawala amesema mara nyingi wanawake wenye maradhi hayo hufika hospitalini wakiwa wamekata tamaa na sonona kutokana na kutengwa na jamii zao na wakati mwingine kupoteza wenza na watoto wao.

“Baada ya matibabu wanawake hao hupelekwa kituo cha “Mabinti Centre” ambako huwezeshwa kimawazo, kijasiriamali na namna bora ya kujiunga tena na familia na jamii zao,” amesema na kuongeza kuwa wanawake 21 wameshapatiwa mafunzo kupitia kituo hicho kwa ufadhili wa Equinor Tanzania.

Mabinti Center ni kituo cha CCBRT cha mafunzo ya ujasiriamali na stadi za maisha kwa wanawake wanaotibiwa fistula na kupona.  Lengo la kituo ni kuwawezesha wanawake hao kiuchumi na kisaikolojia, ili wawe na ujasiri wa kujiunga na jamii na familia zao tena baada ya unyanyapaa na sonona ya muda mrefu iliyosababishwa na kuishi na ugonjwa wa fistula.

Kwa upande wake, daktari bingwa wa magonjwa ya wanawake na upasuaji wa fistula, Peter Majinge amesema hadi leo (Septemba 11), wanawake 20 walikuwa wamefika katika Hospitali ya Sokoine na baada ya uchunguzi, 10 wamegundulika kuwa na fistula ya uzazi, hivyo kuanza kupatiwa matibabu ya upasuaji.

“Tumebaini wanawake 10 wenye fistula ya uzazi, hivyo tunaendelea nao, lakini kambi yetu hii inajumulisha matibabu ya magonjwa mengine ya wanawake hasa yale yanayosababishwa na uzazi kama kutokwa na haja ndogo au kubwa bila kuwa na uwezo wa kujizuia, baada ya kufanyiwa upasuaji wa kuondoa uvimbe au kujifungua.

“Pia tunawahudumia wanaoshindwa kubana hewa kupitia njia ya haja kubwa baada ya kujifungua na kuchanika vibaya msamba sehemu ya uke na haja kubwa wakati wa kujifungua na kushindwa kupata matibabu au kubaki na majeraha ukeni,” amesema Dk Majinge.

Mganga Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Dk Kheri Kagya ameishukuru CCBRT na wadau wake kwa kuendelea kuwajengea uwezo wataalamu wake wa afya ya uzazi mkoani Lindi, ili baada ya kumalizika kwa mradi huo waweze kutoa huduma hiyo katika Hospitali ya Sokoine, kwani hilo ndilo lengo la mradi tofauti na ilivyo sasa ambapo wagonjwa hulazimika kusafiri kwenda CCBRT Dar es Salaam kwa matibabu.

“Kwa kipindi cha hivi karibuni tumeona hatua kubwa za maendeleo katika kuboresha huduma za afya ya uzazi katika mkoa wetu, uimarishaji wa miundombinu ya afya, vifaa vya kisasa na wataalamu wenye ujuzi ambao wanatoa huduma bora kwa wananchi wa Lindi, haya yote yamewezekana kutokana na juhudi kubwa za Serikali kwa kushirikiana na wadau kama hawa wenzetu wa CCBRT na Equinor,” amesema Dk Kagya.


Mnufaika anasemaje?

Saada Hassan (50), mkazi wa wilaya ya Liwale mkoani Lindi, amesema ameteseka na ugonjwa huo kwa takriban miaka 10 kabla ya kupatiwa matibabu.

“Mwezi uliopita nilisikia tangazo redioni likieleza juu ya ugonjwa huu, baada ya kusikiliza vizuri nilibani ndio ugonjwa unaonisumbua, nikachukua namba ya simu waliyotangaza redioni nikaipiga nikaelelezwa kuwa wataalamu wa matibabu ya fistula kutoka Dar Salaam watakuwa hapa kwetu Lindi, sikuamini hadi juzi nilipopigiwa simu na kutumiwa nauli ya kuja hapa hospitalini.

“Nilifika hapa Jumatatu na sasa nimeshapata matibabu, nimeambiwa nikae mpaka Ijumaa, kisha nitaruhusiwa kurejea nyumbani,” amesema na kuongeza;

“Nimeteseka na fistula kwa takribani miaka 10, baada ya kujifungua mtoto wangu wa mwisho. Kipindi hiki kilikuwa na changamoto kubwa, si tu kimaisha bali pia kiroho na kijamii.”

Amesema kwa muda mrefu amekuwa akipambana na hali ngumu, kwani alikuwa akinyanyapaliwa kwa kuitwa majina mabaya kama vile kikojozi.

Takribani wanawake 3,000 wanaugua ugonjwa wa fistula kila mwaka nchini Tanzania.