Waweka kambi kutibu wanawake wenye Fistula
Dar es Salaam. Wakati ikikadiriwa kuwa wanawake 3,000 wanaugua ugonjwa wa Fistula kila mwaka hapa nchini, hospitali ya CCBRT iliyoko Msasani Dar es Salaam na hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Lindi - Sokoine kwa ufadhili wa kampuni ya gesi na mafuta ya Equinor Tanzania, wanaendesha kambi ya utoaji wa matibabu ya Fistula ya uzazi mkoani Lindi.
Kambi hiyo iliyoanza leo inatarajiwa kukamilika Novemba 3, mwaka huu mbali na kutoa matibabu pia inawawezesha akina mama wenye Fistula kiuchumi na kijamii kwa ufadhili wa kampuni ya Equinor inayoiwezesha Serikali na CCBRT kufikia malengo husika.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Jumanne, Oktoba 31, 2023 katika hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Lindi, Meneja wa miradi wa hospitali ya CCBRT Yohana Kasawala, amesema lengo lao ni kuboresha maisha ya wanawake walioathirika na ugonjwa Fistula kwa matibabu wanayowapatia
Amesema hiyo ni awamu ya pili kwa wadau kuendesha kambi hiyo ya matibabu kwani walifanya hivyo Julai 2023 ambapo walitoa matibabu kwa akina mama zaidi ya 30.
“Kimsingi zoezi hili ni endelevu kuanzia mwaka huu wa 2023 hadi 2025, tunalenga kuwafikia akina mama zaidi ya 135 kwa kipindi hicho. Kati ya mwaka 2019 na 2022 tuliwapatia matibabu wanawake 57 kutoka Mkoa wa Lindi walipata matibabu ya Fistula na tuliwapa vifaa vya kujikinga na ugonjwa wa Uviko – 19” amesema
Amesema kupitia ufadhili wa kampuni ya Equinor wameweza kuwatibu na wanawake wenye Fistula, kuwapatia uelewa kuhusu ugonjwa huo na kuwawezesha kiuchumi kupitia mafunzo ya ujasiriamali na stadi za maisha.
Kasawala ameongeza kuwa wanawake 11 kutoka mkoani Lindi waliojiunga katika kituo cha CCBRT cha mafunzo ya ujasiriamali, Mabinti Centre Julai mwaka huu kwa ufadhili wa Equinor watahitimu masomo yao Novemba 17, mwaka huu.
Amesema kituo hicho kinatoa mafunzo kwa akina mama waliougua ugonjwa wa Fistula baada ya kutibiwa kwa lengo la kuwezeshwa kiuchumi ili waweze kurudi katika jamiii zao wakiwa wenye kujiamini na kuendeleza shughuli za uzalishaji mali na kijamii.
“Mara nyingi wanawake hawa hufika hospitali wakiwa wamekata tamaa na sonona kutokana na kutengwa na jamii zao na wakati mwingine kupoteza wenza na watoto wao. Wakiwa katika kituo cha “Mabinti Centre” wanawake hao hupata uponyaji sio tu kwa matibabu ya Fistula bali pia katika kuwezeshwa kimawazo, kijasiriamali” amesema
Kwa upande wake Daktari bingwa wa magonjwa ya akina mama na uzazi hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Lindi –Sokoine, Jamila Athuman alisema ushirikiano na wadau hao umesaidia kuwaongezea ujuzi sambamba na kuwasaidia wagonjwa.
“Muda tunaoshiriki na wenzetu kufanya upasuaji wa fistula ya uzazi nasi tunajifunza ili wakiondoka nasi i tuwe na uwezo wa kufanya wenyewe, hili ni jambo zuri sana kwani tunajifunza kwa vitendo tena tukiwa katika eneo letu la kazi,” amesema