Fistula bado ni janga Tanzania licha ya matibabu bure
Muktasari:
- Tanzania inakadiliwa kuwa na wagonjwa wa Fistula 20,000 na mikoa inayoongoza ni Dar es Salaam, Kigoma, Kagera, Rukwa, Pwani na Tanga
Dar es Salaam. Tanzania inakadiliwa kuwa na wagonjwa wa Fistula 20, 000; huku mikoa inayoongoza ikitajwa kuwa ni Dar es Salaam, Kigoma, Kagera, Rukwa, Pwani na Tanga.
Takwimu hizo zimetolewa leo Alhamisi Julai 13, 2023 na Mganga Mkuu wa Serikali Profesa Tumaini Nagu, wakati wa uzinduzi wa mtandao wa matibabu ya Fistula Tanzania.
Shughuli hiyo iliongozwa na Taasisi ya Fistula Foundation chini ya kauli mbiu ya 'Tuko tayari kuitokomeza' ambapo wameshirikisha wataalamu na madaktari bingwa kutoka hospital 5 zinazotibu ugonjwa huo.
Profesa Nagu amesema kila mwaka inakisiwa wanawake 2000 hadi 3000 wanapata ugonjwa huo lakini wanaofika kwenye matibabu hawazidi 1500.
Amesema licha ya changamoto kubwa ikiyopo lakini nguvu kubwa ikiunganishwa kwa pamoja kati ya wadau na taasisi zinazofanya kazi ya kusaidia waathirika wa ugonjwa huo, hakuna mwanamke ataachwa na akiwa mgonjwa.
"Mtandao huu usaidie kuwafikia wadau wengine ili elimu yetu itawanyike, tusingependa kuona mgonjwa yeyote akiachwa bila matibabu, lazima tuwafuate huko waliko," amesema Profesa Nagu.
Kwa upande mwingine kiongozi huyo ameagiza Fistula Foundation Tanzania kupeleka elimu na kufanya kazi na hospitali zote nchini, wakianzia na hospitali za rufaa ili kila mmoja atambue kuwa ugonjwa huo unatibika.
Meneja Mradi wa Fistula Foundation Tanzania Clement Ndahani amesema matibabu ya ugonjwa huo ni bure na wagonjwa wanaotibiwa wanapona kabisa na kurudi wakiwa wazima hivyo watu wasione haya kujitokeza.
Ndahani amesema baada ya uzinduzi huo, kazi kubwa itakuwa ni kuwatafuta na kuwafikia wagonjwa katika maeneo waliko kwa ajili ya kuwasaidia na kupunguza gharama za kufuatilia matibabu jambo wanaloamini litasaidia kuwaibua wengi.