Matinyi achukua nafasi ya Msigwa kuwa msemaji wa Serikali
Muktasari:
- Rais Samia aendelea kupanga safu ya uongozi baaada ya kumteua Mobhare Matinyi kuwa Msemaji Mkuu wa Serikali akichukua nafasi ya Gerson Msigwa.
Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan ameziba nafasi ya Mkurugenzi wa Idara ya Habari - Maelezo na Msemaji Mkuu wa Serikali kwa kumteua Mobhare Matinyi kushika nafasi hiyo.
Matinyi anachukua nafasi ya Gerson Msigwa ambaye siku chache zilizopita aliteuliwa kuwa Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Utamaduni na Michezo.
Mabadiliko haya yamefanyika ikiwa ni takribani miezi mitatu baada ya Matinyi ambaye kitaaluma ni mwanahabari kuteuliwa kuwa Mkuu wa Wilaya ya Temeke.
Matinyi anakuwa DC mwingine ambaye hajakaa muda mrefu wilayani Temeke akihudumu katika nafasi hiyo kwa siku 87.
Kuondolewa kwa Matinyi Temeke kunafanya hadi sasa kuwe na wilaya tatu ambazo hazina wakuu wa wilaya kutokana na waliokuwepo kuteuliwa katika majukumu mengine.
Wilaya hizo ni Korogwe iliyokuwa ikiongozwa na Jokate Mwegelo ambaye ameteuliwa kuwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Wanawake (UWT) na Wilaya ya Momba iliyokuwa ikiongozwa na Fakii Lulandala aliyeteuliwa kuwa Katibu Mkuu wa UVCCM.