Matokeo ya utafiti yambeba Raila Odinga, Ruto amfuatia

Thursday August 04 2022
marekani pic
By George Helahela

Nairobi. Zikiwa zimesalia siku chache kabla ya kufanyika kwa Uchaguzi Mkuu nchini Kenya, matokeo ya utafiti wa Ipsos na Infotrak yameonyesha mgombea kupitia Azimio la Umoja, Raila Odinga ataongoza dhidi ya mshindani wake wa karibu, Naibu Rais William Ruto wa Kenya Kwanza.

 Matokeo ya Ipsos yanaonyesha kuwa Odinga ataongoza kwa asilimia 47 dhidi ya asilimia 41 za Ruto, huku yale ya Infotrak yanaonyesha Odinga ataongoza kwa asilimia 49 dhidi ya 41 za Ruto.

Katika utafiti uliofanywa na Ipsos umeonyesha kuwa Ruto ameachwa kwa alama sita, huku kampeni zikielekea lala salama.

Ipsos wamesema kuwa matokeo hayo ni matunda ya utafiti uliofanyika kuanzia Julai 23 hadi Julai 26 na pia ukafanyika baada ya mdahalo wa wagombea urais kuanzia Julai 27 hadi Julai 30. Utafiti huo umemtaja mgombea wa tiketi ya chama cha Roots party, George Wajackoyah kushikilia nafasi ya tatu akiwa na asilimia 2.9 za ushindi na David Mwaura akishika mkia kwa kupata asilimia 0.2.

Mkurugenzi wa Ipsos Kenya, Samuel Muthoka alisema kuwa kwenye utafiti huo wamegundua kuwapo kwa asilimia nne ya Wakenya bado hawajaamua watamchagua nani siku ya kupiga kura Agosti 9, mwaka huu lakini kuna uwezekano Odinga akachukua nusu ya kura za watu hao na kumfanya kuwa mshindi wa awamu ya kwanza.

“Kutokana na utafiti huu kama Odinga akiweza kuzibadili nusu ya kura za wananchi ambao bado hawajui watamchagua nani, atakuwa ameweza kupata ushindi kwenye awamu ya kwanza. Lakini ikitokea Ruto ameweza kupata nusu ya kura hizo kutalazimika kurudiwa kwa uchaguzi,” alisema.

Advertisement


Waliohusishwa

Utafiti huo uliofanywa na Ipsos ulihusisha kaya 6,105 kutoka kwenye kaunti zote 47 nchini Kenya na uliwahusisha wapiga kura waliojiandikisha tu na ulihusisha mahojiano ya ana kwa ana huku kiasi cha makosa kikiwa asilimia +- 1.254.

Utafiti huo unaonyesha kwamba waliosema watamchagua Odinga wametoa sababu ya uzoefu, mwanademokrasia na mzalendo wa kweli kwa nchi yake huku waliomchagua Ruto wakieleza kuwa wana matumaini kuwa mgombea huyo ana mipango sahihi itakayowanufaisha Wakenya.

Rais wa Kenya kwenye Uchaguzi Mkuu anapatikana baada ya mgombea kupata kura zaidi ya asilimia 50 ya nchi nzima na angalau apate asilimia 25 ya kura kwenye kaunti 24 kati ya kaunti 47 zinazounda nchi hiyo.

Advertisement