Matukio haya kukumbukwa na IGP Sirro akistaafu polisi

Makamishna wa polisi wakisukuma gari la IGP Mstaafu Sirro wakati wa sherehe ya kumuaga  Mei 10, 2023 kwenye viwanja vya chuo cha mafunzo cha polisi Kurasini. 

Dar es Salaam. Simon Sirro amehitimisha safari ya miaka 30 ya utumishi ndani ya Jeshi la Polisi, huku akisikitishwa na uwepo wa askari ndani ya jeshi hilo wanaokiuka misingi, maadili ya kazi yao na kuwanyonya raia.

Sirro, aliyelitumikia jeshi hilo kuanzia Februari 19 mwaka 1993 na kushika nyadhifa mbalimbali, ikiwemo ya Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP), aliagwa jana katika gwaride maalumu lililofanyika Chuo cha Taaluma cha jeshi hilo Kurasini, jijini Dar es Salaam.

Katika shughuli hiyo ya kuagwa iliyohudhuriwa na askari na maofisa mbalimbali wa jeshi hilo, akiwamo IGP mstaafu Omary Mahita, iliongozwa na Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani, Jumanne Sagini.

Baada ya shughuli hiyo ya kijeshi kukamilika mrithi wake, IGP Camilius Wambura alimkabidhi Sirro kitambulisho cha mstaafu kinachomtambulisha kuwa ni raia wa kawaida.

Akipokea kitambulisho hicho, Sirro alisema: “Nimekabidhiwa kitambulisho cha mstaafu, kwa hiyo mimi ni raia mwema, nataka nipate huduma kutoka polisi”.

IGP Wambura pia alimkabidhi Sirro funguo za gari jipya aina ya Toyota Land Cruiser Prado TX, kama zawadi ya kustaafu kulitumikia jeshi hilo.

Sirro alikaa katika wadhifa huo kwa miaka mitano na mwezi mmoja, tangu alipoteuliwa Mei 28, 2017 na Rais wa awamu ya tano, Hayati John Magufuli akichukua nafasi ya Ernest Mangu.

Alitoka kwenye wadhifa huo Julai 20 mwaka jana, alipoteuliwa kuwa Balozi wa Tanzania nchini Zimbabwe.

Mara baada ya kumaliza kukagua gwaride aliloandaliwa, Balozi Sirro alipanda kwenye gari maalumu na kupita katikati ya askari waliokuwa wamejipanga kama ishara ya kumuaga kijeshi, huku wakati wote akionekana mwenye bashasha.

Gari hilo la wazi lilisukumwa na makamishna waandamizi wa polisi ikiwa ni ishara ya kumuaga rasmi kwenye utumishi wa Jeshi la Polisi ambalo alimaliza kulihudumia katika nafasi ya juu zaidi.
 

…tamu, chungu

Sirro akizungumza na waandishi wa habari kuhusu safari yake ndani ya jeshi hilo, alisema anasikitishwa na askari wanaochafua taswira ya jeshi na kumuachia ujumbe IGP Wambura kulifanyia kazi suala hilo.

Kauli ya Sirro imekuja kipindi ambacho jeshi hilo limekuwa likinyooshewa kidole kwa ukandamizaji wa haki za raia, mauaji, rushwa, vifo vya watuhumiwa wakiwa mikononi mwa polisi na mengine yanayoendana na hayo.

“Jeshi letu linaendeshwa kwa nidhamu, inapotokea baadhi ya askari wanakengeuka inahuzunisha na kuchukiza sana.

“Hili suala nimemwambia IGP Wambura aliangalie sana. Niwakumbushe sisi tupo kwa ajili ya kuwatumikia Watanzania, hatupo kwa ajili ya kutumikiwa na Watanzania,” alisema.

Katika kusisitiza hilo, Sirro alisema: “Ni lazima sisi wenyewe kama askari tuhakikishe tunafanya kazi zetu kwa misingi ya sheria, kanuni na taratibu za Jeshi la Polisi”.

Ushauri huo ulipokewa na IGP Wambura, ambaye alikiri jeshi hilo linahitaji mabadiliko ili kuendana na matakwa ya jamii, huku akieleza suala la maadili ndani ya jeshi hilo linaendelea kushughulikiwa.

“Sasa hivi tupo kwenye maboresho ndani ya Jeshi la Polisi kuanzia kitabia, kiutendaji na mambo mengine. Tunataka tutende kisasa na kiweledi kama jeshi lingine.

“Changamoto kubwa niliyokutana nayo ni ya kimaadili, nidhamu na weledi. Hii ya weledi tunaendelea kuishughulikia kuhakikisha tunapata askari wenye weledi kuanzia wanaoajiriwa na mafunzo kwa waliopo kazini ili kulibadilisha jeshi hili kimtazamo na kiutendaji,” alisema Wambura.

Ushauri huo wa Sirro na maelezo ya IGP Wambura umetolewa kipindi ambacho Tume ya Kupitia Maboresho ya Mifumo ya Haki Jinai iliyoundwa na Rais Samia, ikiendelea kukusanya maoni jinsi ya kuziboresha, ikiwemo Jeshi la Polisi.
 

Aliyokabiliana nayo

Sirro alisema akiwa IGP alikutana na mambo kadhaa yaliyokuwa changamoto, lakini jeshi hilo lilisimama kikamilifu kuhakikisha usalama wa raia na mali zao unaendelea kuwepo nchini.

Akitolea mfano wa mambo hayo, alisema ni matukio ya unyang’anyi kwa kutumia silaha, tukio la mauaji ya Kibiti, mkoani Pwani, hofu ya wafanyabiashara kufanya biashara zao usiku na changamoto ya panyarodi. “Mtakuwa mnakumbuka kuna kipindi matukio ya unyang’anyi kwa kutumia silaha yalishika kasi mchana kweupe nikasema hapana, lazima tukomeshe na kweli tulifanikiwa.

“Pia, hali ilivyokuwa Kibiti hadi viongozi wakawa hawawezi kwenda kule, zamani kulikuwa hakuna biashara usiku lakini siku hizi maduka yako wazi hadi usiku,” alisema Sirro, aliyezaliwa Machi 29, 1963 katika kijiji cha Kiabakari mkoani Mara.

Kuhusu matukio ya watu kutekwa na kupotea alisema: “Unapokuwa mkuu wa Jeshi la Polisi suala la ulinzi na usalama wa raia na mali zao ni muhimu, hivyo yanapotokea matukio ya uhalifu, ikiwemo watu kutekwa au kupotea IGP huwezi kuwa sawa.

“Kinachofanyika hapo ni kutafuta nani kafanya, maana kama umeshindwa kuzuia ni lazima uweke nguvu ya kuwapata wahusika.

“Kuna matukio tuliwapata wahusika, mengine hatukuwapata kwa sababu ni suala la upelelezi, unaweza kufanikiwa au usifanikiwe na Watanzania waelewe si kila tukio likifanyika polisi anaweza kubaini,” alisema Sirro.

Sehemu ya matukio katika maisha yake ya kazi, ikiwemo ya utekaji na watu kupotea

Baadhi ya matukio ya utekaji ni la Oktoba 2017 la Ben Saanane, msaidizi wa Freeman Mbowe wa Chadema alipotea na hadi sasa hajulikani alipo. Lingine ni la Novemba 21, 2017 likimhusu mwandishi wa habari wa gazeti la Mwananchi, Kibiti, Azory Gwanda aliyechukuliwa na watu wasiojulikana. Hadi sasa hajapatikana.

Oktoba 19, 2018: Alisema kamera zimesaidia polisi kutambua gari lililohusika katika tukio la kutekwa mfanyabiashara maarufu Mohammed Dewji na wamemtambua dereva na namba ya gari lililotumika katika tukio hilo. Februari 16, 2018: Mwanafunzi wa Chuo cha Usafirishaji (NIT), Akwilina Akwilini aliaga dunia baada ya kupigwa risasi na polisi wakati wa uchaguzi jimbo la Kinondoni. Tukio hilo lilitokea eneo la Mkwajuni, Kinondoni, Dar es Salaam.
 

Tukio ambalo hatalisahau

Katika miaka sita aliyotumikia nafasi ya IGP ameweka wazi kamwe hawezi kusahau tukio la mauaji lilitokea wilayani Kibiti Aprili 13 mwaka 2017 ambako askari tisa waliokuwa na silaha wakitokea lindo walivamiwa na kuuawa kisha kunyang’anywa silaha.

“Tukio ambalo siwezi kulisahau ni lile lililotokea Kibiti, askari tisa tena walikuwa vijana wadogo, wanatoka lindo wakapigwa ambush na kunyang’anywa silaha,” alisema na kuongeza:
“Ukiwa kiongozi wa jeshi halafu kukuta askari tisa wamelala kwa kupigwa risasi si jambo dogo. Hata hivyo, tulipambana kuwapata wahusika ambao bahati mbaya na wao walitangulia mbele ya haki, ila tulifanikiwa kurejesha silaha zetu zote”.

Nyongeza na William Shao