Matumizi holela antibiotiki kwa wanyama na athari kwa walaji

Meneja wakala ya maabara ya veterinari Tanzania kanda ya nyanda za juu kusini Dr Qwari Bura akizungumza katika uzinduzi wa maadhimisho ya miaka 10 ya TVLA.
Muktasari:
- Inakadiriwa kufikia mwaka 2030 watu zaidi ya milionni watakufa kila mwaka kutokana na dawa kushindwa kuwatibu kwani vimelea vya magonjwa vitakuwa vimejenga usugu unaotokana na matumizi holela ya dawa kwa binadamu na mifugo.
Iringa. Inakadiriwa kufikia mwaka 2030 watu zaidi ya milionni watakufa kila mwaka kutokana na dawa kushindwa kuwatibu kwani vimelea vya magonjwa vitakuwa vimejenga usugu unaotokana na matumizi holela ya dawa kwa binadamu na mifugo.
Kauli hiyo imetolewa leo Jumanne Novemba 22, 2022 na Meneja wa wakala ya Maabara ya Veterinari Tanzania kanda ya nyanda za juu kusini Dr Qwari Bura wakati akizindua wiki ya maadhimisho ya miaka kumi ya TVLA mkoani Iringa.
Novemba 19, 2022, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Dk Seif Shekalaghe amesema katika utafiti uliofanyika mwaka 2018, ulionesha asilimia 90 ya wafugaji wanatumia dawa za antibiotiki kutibu wanyama badala ya chanjo, hivyo kusababisha ongezeko kubwa la usugu wa Vimelea dhidi ya dawa za antibiotiki.
Dk Bura amesema kuna umuhimu mkubwa wa kupima na kujua ugonjwa unaomsumbua mnyama ili kutoa tiba sahihi kwani husaidia kuondoa tatizo la kutibu kwa majaribio jambo ambalo husababisha mfugaji kutumia dawa aina nyingi zinazoweza kusababisha usugu wa vimelea vya magonjwa dhidi ya dawa.
“Matumizi holela ya dawa hasa antibiotiki huweza kuathiri binadamu kutokana na kula mabaki ya dawa hizo kwenye vyakula vitokanavyo na wanyama,” amefafanua.
Amesema hilo limekuwa ni tatizo kubwa linaloikabili dunia kwa sasa na wafugaji wanapaswa kuzingatia ushauri na wataalamu ili kudhibiti tatizo hilo.
Dk Bura ameeleza wafugaji wanapaswa kuacha mara moja kutibu wanyama wao bila vipimo ili kulinda afya ya wanyama na binadamu
“Tunawashauri wafugaji kuacha kuwatibu mifugo holela bila kuwapima na kutumia dawa za antibiotiki bila utaratibu kwani ni hatari kwa afya ya binadamu anayekula mnyama huyo,” amesema.
Amesema wakala ya maabara ya Veterinari Tanzania imejipanga kutoa chanjo ya ugonjwa wa mdondo kwa kuku bure kwa kuwa ni mkombozi wa wafugaji wa maeneo yote mjini na vijijini.
Amesema katika kuwasaidia watengenezaji wa vyakula vya mifugo kuweza kutengeneza vyakula bora ambavyo vinatoa lishe kamili kwa Wanyama,wakala imfanikiwa kuongeza uwezo wa kupima aina na kiwago cha madini kilicho katika vyakula vya mifugo.
“Katika kulinda binadamu dhidi ya adui maradhi maabara za rufaa za wakala zimekuwa zikishiriki katika uchunguzi wa mlipuko wa magonjwa yanayoathiri Wanyama na binadamu kama vile kimeta, kichaa cha mbwa, ugonjwa wa kutupa mimba, malale, na homa ya mgunda,” amesema.
Kwa upande wake, mmoja wa wafugaji katika mtaa wa Kihesa Mkoani Iringa, Jonathan Kilale amesema kuwa wakulima na wafugaji wengi hawana elimu ya kutibu mifugo yao hivyo hukisia maradhi na kuwapa dawa.
“Ikitokea kuku wangu wakaugua huwa naenda tu duka la madawa ya mifugo na kujieleza nakupewa dawa bila kuonana na dakitari wa mifugo unakuta wakati mwingine nikitumia dawa hizo kuwapa kuku wanakufa kwa wingi bila kujua tatizo ni nini,” amesema.
Naye Doris Mvela amesema kuwa kutokana na kukosa elimu watu wengi wamekuwa wakiwalisha miugo vyakula visivyofaa ili wanenepe na kukua kwa haraka ili waweze kuwaingiza sokoni bila kujari athari zitakazo mpata mtu atakaye kula mnyama huyo.