Matumizi viuatilifu bila elimu yanavyohatarisha afya za wakulima

Matumiziviuatilifu bila elimu yanavyohatarisha afya za wakulima

Muktasari:

Kampuni ya viuatilifu ya Mo Green imesema wakulima wengi wamejiweka kwenye hatari ya kupata athari za kiafya kutokana na matumizi yasiyo sahihi ya viuatilifu ikiwemo kupiga dawa bila vifaa vya kujikinga.

Mbeya. Wakulima wanaotumia viuatilifu bila kuwa na elimu ya upigaji wa dawa kwenye mazao yao pamoja na vifaa vya kujikinga wapo hatarini kupata madhara kiafya.

 Akizungumza na Mwananchi leo Jumamosi Agosti 6, 2022 katika maonyesho ya sherehe za wakulima ya Nanenane yanayoendelea Jijini Mbeya, Afisa Kilimo wa Kampuni ya Mo Green, Alex Michael amesema utafiti wao unaonyesha wakulima wengi hawana elimu ya upigaji wa viuatilifu kwenye mazao yao.

Amesema yapo baadhi ya magonjwa yanayoweza kupatikana ikiwamo saratani ngozi, saratani ya kizazi, msongo wa mawazo, matatizo ya mfumo wa neva, mimba kutoka, kupata watoto wenye ulemavu na magonjwa mengine.

“Wakulima wengi wamejisababishia madhara ya kiafya kutokana na matumizi ya viuatilifu bila kujikinga au kuvaa vifaa maalum, hii ni kwa sababu hawana maarifa,” alisema.

Alisema kutokana na hali hiyo, pamoja na kuuza viuatilifu wamekuwa wakitoa elimu ya namna ya kupiga dawa na kuwashauri wakulima wajiunge kwenye vikundi ili wapate vijana watakaowapeleka kwenye mafunzo rasmi ya upigaji wa dawa.

“Sio rahisi mkulima mmoja mmoja kwenda kupata haya mafunzo, Me Green tunawashauri wajiunge tu kwenye vikundi, wateue watu hasa vijana na hawa watakuwa wakifanya kazi hii kwa umakini bila kujisababishia madhara,” alisema.

Alisema madhara mengi hutokea baada ya muda mrefu jambo ambalo wengi huwa hawajui sababu za kupata magonjwa haya.

“Kwa mwanzo anaweza kuhisi miasho tu ukachukulia kawaida, lakini baadae ni hatari sana,” alisema Michael.

Alisema mbali na kutovaa vifaa, changamoto nyingine wanazokutana nazo wa kulima wakati wa kupiga dawa ni kukosa elimu ya dawa gani waitumie kwa wakati gani na vipimo jambo ambalo pia linaweza kuathiri upatikanaji wa mazao ya kutosha.

“Kwa hiyo huduma za maafisa ugani kwa wakulima ni muhimu sana kama ilivyo kwa binadamu, huwezo kutibiwa bila kujua aina ya ugonjwa na dawa gani utumie kwa muda gan,” amesema Michael.

Amesema pamoja na usambazaji wa viuatilifu kwa wakulima, baada ya kubaini changamoto hizo waliamua kuanzisha huduma ya kutoa elimu kwa wakulima.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Mo Green, Matolo Felician amesema changamoto zinazowakabili wakulima kwenye matumizi sahihi ya viuatilifu ndizo zilizomsukuma kuanzisha kampuni hiyo.

“Tunataka mkulima apate pembejeo na viutatilifu rafiki vinavyoweza kumsaidia katika kutatua changamoto yake ya kupatikana kwa mazao bora. Tumejikita kwenye mazao ya Pamba, Korosho na Tumbaki,” amesema.

Amesema ili kilimo kiwe biashara na kuweza kuifikia ajenda ya 10/30 lazima wakulima wapewe elimu ya matumizi sahihi ya pembejeo vinginevyo wataendelea kulima mazao mengi lakini bila tija.

“Wakulima wasilime kwa mazoea, walime kibiashara kwa kufuata misingi na miongozo yote ya kilimo, sisi tulipita kijiji kwa kijiji mkoani Mtwara tulipta kijiji kwa kijiji tukagundua changamoto ambazo tunafanyia kazi,” amesema.

Kwa upande wao baadhi ya wakulima wameshauri Serikali kusimamia na kuhakikisha wauzaji wa vifaa vya kilimo hasa pembejeo na viuatilifu wanakuwa na elimu ya ugani ili kuwasaidia katika kuwapatia elimu.

“Sasa unaenda dukani unagundua afisa muuzaji mwenyewe hajui chochote, unatumia uzoefu kununua dawa mwisho unapata madhara kwa mazao yako kuharibika. Kama Waziri Ummy alivyofanya kwenye afya, Waziri Bashe nae afanye kwenye kilimo ili tufikie ajenda ya 10/30,” amesema.