Kilimo mseto kinavyoweza kumpunguzia gharama mkulima

Kilimo mseto kinavyoweza kumpunguzia gharama mkulima

Muktasari:

  • Wakulima wameshauriwa kulima kilimo mseto kinachojumuisha pamoja ufugaji wa samaki, kuku na bustani ya mbogamboga

Mbeya. Wataalamu wa kilimo wamesema kilimo mseto kinacho jumuisha pamoja ufugaji wa samaki, kuku na bustani ya mbogamboga kinaweza kumpunguzia mkulima gharama za uwekezaji.

 Kupitia kilimo hicho, mkulima akichimba bwawa la samaki, anatakiwa kujenga mabanda ya kuku juu yake ambayo yatasaidia chakula cha samaki kupitia kinyesi na mabaki ya chakula huku maji yake yakitumika kumwagilia bustani.

Akizungumza katika banda la Halmashauri ya Wilaya ya Mbozi, Mtaalamu wa Kilimo, Marine Kimathy amesema faida ya kilimo hicho kupunguza gharama ya uwekezaji, matumizi bora ya ardhi na kuongeza lishe kwenye familia.

“Binafsi nalima kilimo hiki, nina uhakika wa kupata samaki, mboga za majani, mayai na kuku katika eneo dogo sana,” amesema

Amesema mabanda ya kuku yakijengwa ndani ya bwawa la samaki huachwa nafasi ili kinyesi cha kuku na mabaki ya chakula yamwagikie kwenye bwawa hilo.

Alisema vitu hicho vinapomwagika kwenye bwawa la samaki huwa chakula kizuri na baadae, maji yake hupata mbolea ambayo yakitumika kumwagilia mbogamboga kurutubisha ardhi.

“Hii ni teknolojia nyingine inayoweza kumfanya mkulima akapata faida nyingi kwa wakati mmoja na kwa gharama naafuu kabisa,” amesema.

Mtaalamu mwingine, Frank Mbunda alisema kilimo hicho kinaweza kutumika kama njia ya kupambana na utapiamlo hasa kwenye mikoa inayoongoza kwa tatizo hilo ikiwamo Mbeya, Iringa na Njombe.