Mauaji yatikisa Kilimanjaro

Wednesday October 13 2021
mauajipicc
By Waandishi Wetu

Ni mtikisiko, hivi ndivyo unavyoweza kuelezea wimbi la mauaji linaloendelea mkoani Kilimanjaro kutokana na ulipizaji kisasi, migogoro ya kifamilia na ardhi na kwa miezi tisa pekee, watu 12 wameuawa.

Matukio ya hivi karibuni ambayo yamethibitishwa na Kamanda wa Polisi mkoani Kilimanjaro, Simon Maigwa ni la kuuawa kwa mtoto mdogo mwenye umri wa miaka 6, kuuawa kwa mwenyekiti wa kijiji na mauaji ya mkazi wa Kilema.

Mauaji hayo yametokea kati ya Februari 2021 hadi Oktoba 10, 2021 katika maeneo mbalimbali ya Mkoa wa Kilimanjaro, huku baadhi ya matukio wauaji wakiwa wamekodiwa kwa kati ya Sh300, 000 na Sh400, 000.

Tukio la Oktoba 10, ndio limeacha simanzi kubwa baada ya mtoto mdogo mwenye umri wa miezi 6, kuchinjwa kwa kukatwa shingo na mtuhumiwa ambaye ni baba yake mdogo anayedhanikiwa kuwa na matatizo ya akili.

Mbali na tukio hilo, Oktoba 5, 2021, Mwenyekiti wa kijiji cha Kombo, Kata ya Kibosho Magharibi, wilayani Moshi,Joachim Sakaya aliuawa kwa kukatwa katwa mapanga na kisha mwili wake kutupwa shambani.

Pia Septemba 26, 2021, Mkazi wa kijiji cha Makami Juu, Kata ya Kilema Kaskazini wilayani Moshi, Gaspar Mremi (58) aliuawa na watu wanaodaiwa kukodiwa kwa Sh300, 000 ili kulipiza kisasi kwa kumpiga baba yake.

Advertisement

Mwenyekiti wa kijiji hicho, Kornel Lyamuya alisema tukio hilo lilitokea baada ya marehemu kumpiga baba yake mzazi, Aloyce Mremi na fimbo kichwani na ndipo mmoja wa wana ndugu alipokodi wauaji hao.

“Marehemu ana tatizo la akili. alimpiga baba yake na fimbo kichwani sasa mtoto wa mke mdogo ndiye aliyesema aliyempiga baba yake auwawe. Taarifa zilizopo zilitumwa Sh300, 000 kwa simu ili kukodi watu wampige”alisema Lyamuya.

alisema baada ya tukio hilo alipigiwa simu kujulishwa kuhusu kupigwa kwa marehemu na watu wanaofahamika na alipofika eneo la tukio alimkuta anavuja damu na hajiwezi na baadaye alifariki.

Kauli ya RPC

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Simon Maigwa alithibitisha kutokea kwa mauaji hayo, na kueleza kuwa jeshi hilo linawashikilia watu 7, wanaodaiwa kuhusika na matukio hayo matatu ya mauaji ya hivi karibuni.

Akizungumzia tukio la kuchinjwa kwa mtoto wa miezi 6, Kamanda Maigwa alisema mtoto huyo alikuwa akiishi na bibi yake na siku hiyo mtuhumiwa anadaiwa pia alimkata ndama kwa panga na kumuua.

“Mtuhumiwa alichukua panga linalotumika kukatia majani ya ng’ombe alimkata ndama shingoni na kufa papo hapo, kisha kwenda kumkata shingoni na kitu chenye ncha kali mtoto wake na kutenganisha kichwa na kiwiliwili,” alisema.

Kuhusu kuuawa kwa Mwenyekiti wa Kijiji wilayani Moshi, Kamanda Maigwa alisema wamewakamata watu watatu na uchunguzi zaidi bado unaendelea kuhusiana na tukio hilo.

“Tukio hili linahusishwa na migogoro ya ardhi na mambo ya kifamilia, kuna mambo ambayo hatuwezi kuyazungumza kwa sababu ya uchunguzi, lakini tutatoa taarifa tutakapokamilisha uchunguzi,” alisema Kamanda Maigwa.

Kuhusu tukio la mauaji ya Kilema, alisema Jwanawashikilia watu watatu ambao tayari wamekiri kwa mlinzi wa amani kuhusika na mauaji hayo na taratibu zikikamilika watafikishwa mahakamani.

Alieleza kuwa katika matukio mengi ya mauaji yanayotokea mkoani humo vyanzo vyake ni migogoro ya ardhi, familia kwa familia, matumizi ya dawa za kuleva na ulevi.

“Niitake jamii kuliangalia hili, kama shida ni ardhi yapo maeneo ipo ya kutosha waende huko waache kugombana, lakini pia zipo kamati za ardhi kuanzi ngazi za vijiji na kata, wafike huko wakapate suluhu,” alisema.

Kamanda Maigwa alitumia aliitaka jamii kushirikiana na jeshi hilo kutokomeza matukio ya uhalifu, kwa kuwa polisi ni wachache hivyo hawawezi kwenda, kujua mambo ya kila eneo.

DC Moshi atoa neno

Mkuu wa Wilaya ya Moshi, Said Mtanda ambaye aliwataka wananchi wa Kilimanjaro kujenga utamaduni wa maridhiano pale migogoro inapotokea katika familia.

Alisema kufanya hivyo kutaepusha madhara ambayo yanayoweza kutokea ikiwemo kudhuriana au kusababisha kifo kama ambavyo sababu za baadhi ya mauaji zinajieleza.

“Wananchi wanatakiwa kumuamini Mungu kwa imani zao, na hakuna sababu ya kupigana au kuua binadamu mwenzako maana hakuna faida yoyote zaidi ya kwenda polisi na kushtakiwa,”alisema Mtanda.

Matukio mengine yaliyotikisa

Februari 9, 2021, Magreth Mushi (50), mkazi wa kijiji cha Urauri wilayani Rombo, aliuawa kwa kukatwa mapanga na mtuhumiwa ambaye ni ndugu yake wakigombea fedha zilizotokana na mauzo ya nyanya za marehemu.

Mbali na tukio hilo, Aprili 17 mkazi wa Kijiji cha Muwara Kata ya Makiwaru wilayani Siha, Magdalena Makishe (61) aliuawa kwa kile kilichodaiwa ni ugomvi wa kifamilia na anayedaiwa kuwa ni mumewe.

Lakini mwezi huo huo, katika kijiji cha Uria, Kata ya Kahe, mtoto wa miezi 9, Elikarimu Furaha aliuawa na baba yake aitwaye Elifuraha Mlay (23) kisha naye kujiua kwa kujinyonga.

Mei 31, 2021, askari polisi aitwaye Linus Nzema wa kituo cha Polisi Mwanga aliuawa kwa kupigwa risasi nje ya baa iitwayo Ndafu iliyopo kijiji cha Kituri, baada ya kutokea kuzozana na askari mwenzake waliokuwa wote doria.

Mbali na hilo, Juni 2021, mlinzi wa Suma JKT, Emmanuel Mallya alidaiwa kuuawa kwa kupigwa risasi nyingi mwilini akiwa lindo kituo cha kupooza umeme cha Kiyungi.

Julai 12, Mkazi wa kijiji cha Challa wilayani Rombo, John Kavishe (77) anadaiwa kumuua mwanaye Andrew Kavishe (31) kwa kumkata panga shingoni wakati akisuluhisha mgogoro wa kifamilia.

Pia Agosti 30, Elice Matafu mkazi wa kijiji cha Mrimbo Uwo, kata ya Mwika wilayani Moshi ambaye ni mke wa mfanyabiashara Patrice Matafu, aliuawa kwa kuchinjwa na watu wasiojulikana akiwa nyumbani kwake.

Septemba 10, Elizabeth Shayo (63) mkazi wa Himo darajani wilayani Moshi, aliuawa kikatili na vijana wanne ambao taarifa zilizozagaa katika mji wa Himo, ambazo hazijathibitishwa zinadai kuwa walikodishwa kwa kulipwa Sh400, 000 kufanya mauaji hayo.

Septemba 17, Mwanaidi Hamis, mkazi wa Kijiji cha Ngulu, Kata ya Kwakoa wilayani Mwanga, anadaiwa kuuawa kwa kuchinjwa na panga kutokana na kile kilichoelezwa ni wivu wa mapenzi.


Habari hii imeandikwa na Daniel Mjema, Florah Temba na Fina LyimoAdvertisement