Mauaji yatikisa wilayani Serengeti

Mauaji yatikisa wilayani Serengeti

Muktasari:

  • Watu sita  wamefariki  baada ya kujeruhiwa na  visu na mapanga katika matukio tofauti yaliyotokea katika Wilaya ya Serengeti mkoani Mara.


Serengeti. Watu sita  wamefariki  baada ya kujeruhiwa na  visu na mapanga katika matukio tofauti yaliyotokea katika Wilaya ya Serengeti mkoani Mara.

Matukio hayo yametokea  katika kipindi cha miezi mitatu katika  maeneo ya sterehe.

Azikungumza mjini Mgumu leo Jumanne Septemba 21, 2021 katika uzinduzi wa ofisi ya Taifa ya mashtaka ya Wilaya ya Serengeti, mkuu wa wilaya hiyo, Dk Vicent  Mashinji amesema  zipo hatua mbalimbali zilizochukuliwa na uongozi wa wilaya  kuhakikisha matukio ya mauaji yanapungua katika wilaya hiyo.

Amesema  hatua hizo ni pamoja na kupiga marufuku ubebaji wa visu  na mapanga  katika sehemu za starehe kwa maelezo kuwa wenye silaha hizo imeelezwa kuwa muda wowote wanaweza kutekeleza mambo maovu.

"Tumegundua  ubebaji holela wa mapanga na visu katika sehemu za starehe ni kichocheo cha matukio haya kwani kuna watu wanashindwa kuhimili kiwango cha kilevi,  wanafikia hatua ya kutumia silaha hizo kudhuru na hata kuua pale inapotokea wametofautiana kauli, " amesema.

Amesema  kutokana na ubebaji huo holela wa silaha,  matukio ya mauaji katika Wilaya ya Serengeti yamekuwa mengi hali inayotakiwa kukomeshwa.

Amebainisha uwepo wa  ofisi hiyo utasaidia mapambano ya mimba za utotoni wengi wakiwa wanafunzi.

Mkurugenzi mkuu wa Mashtaka nchini(DPP),  Sylvester Mwakitalu amesema  hadi kufikia Septemba 10,  2021 wilaya ya Serengeti ilikuwa na kesi 29 za mauaji ambapo kesi 25 ni za mauaji ya kukusudia huku kesi nne zikiwa ni za mauaji ya bila kukusudia.