Maudhui ya ukatili kwa watoto sasa marufuku Youtube

Muktasari:

Jukwaa la mtandaoni la YouTube haliitaruhusu maudhui yanayoigiza kwa uhalisia watoto waliofariki au walioathiriwa na matukio ya ukatili wa kijinsia baada ya kuhuisha sera yake.

Dar es Salaam.  Inawezekana ukawa miongoni mwa watu wanaochukizwa na maudhui ya ukatili kwa watoto.

Habari njema ni kwamba, jukwaa la maudhui mtandaoni la YouTube halitaruhusu tena maudhui yanayoigiza kwa uhalisia watoto waliofariki au walioathiriwa na matukio ya ukatili wa kijinsia.

Jukwaa hilo la video limehuisha sera yake ya unyanyasaji na udhalilishaji mtandaoni ili kupiga marufuku maudhui ya aina hiyo, yakiwa yamerekedi matukio kuelezea vifo vyao au unyanyasaji wao.

Kwa mujibu wa mtandao wa Cybernews, Google inayomiliki YouTube imesema sera itaanza kutumika Januari 16, 2024.

“Ni sehemu ya juhudi zake za uwajibikaji ambazo hapo awali zilijumuisha kupiga marufuku maudhui kuhusu chanjo ya Uviko-19 iliyopingana na makubaliano kutoka kwa mamlaka ya afya na kutumia kanuni ya kuweka vikwazo vya umri kwa video husika,” imesema taarifa hiyo ya Youtube.

Mabadiliko ya sera hiyo yanakuja baada ya kusambaa video za uhalifu kwenye majukwaa ikiwamo TikTok na YouTube zinazoonyesha mfano wa watoto waliokufa au kupotea. 




Baadhi ya video hizo zilitumia picha zilizotengenezwa na akili bandia (AI) za James Bulger, mtoto Mwingereza mwenye umri wa miaka miwili aliyetekwa nyara na kuuawa mwaka  1993.

Pia, kuna video za Madeleine McCann, msichana wa miaka mitatu wa Uingereza ambaye alitoweka nchini Ureno mwaka 2007. 

Tayari TikTok ilishaanza kuondoa video hizo ikifafanua: “Mwongozo wetu wa jumuiya ni wazi kwamba haturuhusu maudhui ya aina hiyo.”