Prime
Maumivu ya ukatili wa kijinsia yamgeuza kuwa mkombozi
Mwalimu Veronica Kidemi ambaye pia ni mwanzilishi wa Taasisi isiyokuwa ya Kiserikali ya Voice of Women Africa, (aliyevaa fulana nyeusi) akimwelekeza mmoja wa wananchi wa Wilaya ya Serengeti, Mara namna ya kutumia mkono bandia, hivi karibuni alipokwenda kutoa mikono hiyo kwa jamii.
Muktasari:
- Mwalimu Veronica Kidemi, aliyepoteza mkono wa kulia baada ya kukatwa na aliyekuwa mumewe mwaka 2020 kutokana na ukatili wa kijinsia, anasema ukimya wa waathirika huchangia madhara makubwa zaidi.
Arusha. Miaka sita iliyopita, Mwalimu wa Shule ya Sekondari Sokoni II, Veronica Kidemi, alikuwa akiishi katika ndoa iliyogubikwa na ukatili wa kijinsia na mateso ya muda mrefu, hali iliyomfanya kunyamaza kwa muda mrefu akiamini mambo yangebadilika.
Hata hivyo, ukimya huo uliishia katika tukio la kushtua mwaka 2020, baada ya aliyekuwa mumewe kumkata mkono wa kulia, tukio lililobadilisha kabisa maisha yake ya kila siku na taaluma yake ya ualimu.
Akizungumza katika mahojiano maalumu na Mwananchi jijini Arusha, Veronica anasimulia safari ya maumivu, mapambano na hatimaye mafanikio, akitoa wito kwa wanawake wanaokumbwa na ukatili kutokaa kimya.
“Nilipopoteza mkono wangu wa kulia Septemba 2020 nilishtuka sana. Niliwaza nitaendeleaje kufundisha wakati kazi yetu kubwa ni kuandika na kuwasiliana darasani,” anasema.
Akiwa bado hospitalini, Veronica alichukua uamuzi wa kuanza upya maisha kwa kujifunza kuandika kwa mkono wa kushoto. Akiwa hospitali aliiomba daftari na kalamu na kuanza mazoezi ya kujifunza upya uandishi.
“Siku za mwanzo zilikuwa ngumu sana. Nilikuwa nachanganya herufi, maandishi hayaeleweki na mkono ulikuwa dhaifu, lakini nilijua sina njia nyingine zaidi ya kupambana,” anasema.
Anasema aliendelea na mazoezi ya kuandika sambamba na tiba ya viungo hadi mkono wake wa kushoto ulipopata nguvu na kumwezesha kurejea katika shughuli zake za kazi.
Leo, Veronica anasema anaendelea kufundisha kwa ufanisi na amekuwa miongoni mwa walimu wanaofanya vizuri katika halmashauri yake, hali anayoitaja kuwa uthibitisho kwamba ulemavu hauzuii mafanikio.
“Tangu nipate ulemavu, nimekuwa miongoni mwa walimu bora. Mara mbili nimeingia katika nafasi za juu kwa matokeo ya kidato cha nne na nimepata vyeti vya pongezi,” anasema.
Mbali na mafanikio ya kitaaluma, Veronica alichaguliwa miongoni mwa walimu wanne kati ya zaidi ya 440 nchini kushiriki programu ya kubadilishana uzoefu nchini Marekani, ambako alitembelea Chuo Kikuu cha Georgia State jijini Atlanta na baadaye kukamilisha mafunzo yake mjini Washington, D.C.
Anasema uzoefu alioupata, pamoja na maumivu aliyopitia, ulimchochea kuanzisha taasisi ya Voice of Women in Africa, inayolenga kupinga ukatili wa kijinsia na kusaidia watu wenye ulemavu.
Kupitia ushirikiano na The Hand Project ya Ujerumani, taasisi hiyo imefanikiwa kutoa mikono bandia zaidi ya 700 kwa watu mbalimbali nchini.
“Nilipoteza mkono na nikajua maumivu yake. Nikajua pia changamoto na aibu anayopitia mtu mwenye ulemavu. Hilo ndilo lililonisukuma kusaidia wengine,” anasema.
Anasema asilimia kubwa ya waliopoteza viungo waliosaidiwa kupitia mpango huo wameathiriwa na ukatili wa kijinsia, hali iliyomshtua kuhusu ukubwa wa tatizo hilo katika jamii.
“Zaidi ya asilimia 80 ya watu tuliokutana nao walipoteza viungo kutokana na ukatili. Hilo liliniumiza sana,” anasema.
Mwalimu Veronica Kidemi ambaye pia ni mwanzilishi wa Taasisi isiyokuwa ya Kiserikali ya Voice of Women Africa, (aliyevaa fulana nyeusi) akiwaelekeza wanufaika wa mikono bandia namna ya kutumia mikono hiyo kufanya kazi, katika Hospitali ya Wilaya Serengeti mkoani Mara hivi karibuni
Veronica anaamini kuwa mfumo wa kisheria unapaswa kuimarishwa ili kuhakikisha waathirika wa ukatili wanapata haki na fidia kwa wakati, badala ya kubebeshwa gharama za matibabu peke yao.
“Ninaamini anayesababisha madhara anapaswa kuwajibika moja kwa moja kugharamia matibabu na mahitaji ya mwathirika,” anasema.
Anasema kosa kubwa alilofanya ni kunyamaza kwa muda mrefu alipokuwa akipitia mateso ya ndoa, akisisitiza kuwa ukimya unaweza kusababisha madhara makubwa zaidi.
“Wanawake wengi wanaogopa kuzungumza, lakini ukimya unaweza kulipuka na kuwa janga kubwa,” anasema.
Anawahimiza wanawake na wasichana wanaokumbwa na ukatili kutoa taarifa mapema kwa familia, viongozi wa jamii, dawati la jinsia na watoto na mamlaka husika.
“Ukatili si jambo la kufumbia macho. Kuna ukatili wa kisaikolojia, wa maneno na wa kimwili. Usinyamaze,” anasema.
Wakati huo huo, Chama cha Wanasheria Wanawake Tanzania (TAWLA) Mkoa wa Arusha kimeendesha mafunzo kwa wadau wa mnyororo wa haki jinai kuhusu kushughulikia kesi za ukatili wa kijinsia.
Mratibu wa TAWLA Mkoa wa Arusha, Neema Ahmed, anasema mafunzo hayo yaliwakutanisha watendaji wa kata, maofisa maendeleo ya jamii, ustawi wa jamii, polisi wa dawati la jinsia na watoto pamoja na waendesha mashtaka.
Anasema lengo lilikuwa kuimarisha ushirikiano na kuboresha utoaji wa haki kwa waathirika wa ukatili wa kijinsia, kuanzia hatua ya kutoa taarifa hadi kesi inapofikishwa mahakamani.
Kwa mujibu wake, changamoto kubwa ni ukosefu wa ushirikiano wa wananchi, baadhi ya waathirika kuhama maeneo yao na mila potofu zinazochangia baadhi ya kesi kusuluhishwa nje ya mfumo wa sheria.
Mkuu wa Dawati la Jinsia na Watoto Wilaya ya Arumeru, Inspekta Salama Ally, anasema ushirikiano wa wadau ni muhimu katika kuhakikisha waathirika wanapata haki na kupunguza ukatili katika jamii.
Anasema elimu kwa jamii na ufuatiliaji wa karibu wa kesi ni muhimu katika kufikia jamii isiyo na ukatili wa kijinsia.
Wadau hao wanahimiza utoaji wa elimu ya mara kwa mara kwa jamii, ushirikiano wa taasisi na uhamasishaji wa kutoa taarifa mapema kama njia ya kupunguza na hatimaye kutokomeza ukatili wa kijinsia nchini.