Mawakili Chadema kuwahoji wabunge wawili kesi ya kina Mdee
Muktasari:
Mahakama Kuu imeridhia ombi la kuitwa mahakamani kwa wabunge Grace Tendega na Hawa Mwifunga Septemba 30 ili awahojiwe na mawakili wa Chadema.
Dar es Salaam. Mahakama Kuu imepanga Septemba 30, 2022 kuanza kusikiliza kesi iliyofunguliwa na Mbunge wa viti Maalum (Chadema), Halima Mdee na wenzake 18.
Mahakama hiyo pia imeridhia ombi la kuitwa mahakamani Mbuge Grace Tendega na Hawa Mwifunga wafike tarehe hiyo ili wahojiwe na mawakili wa wajibu maombi wa kwanza ambao ni Chadema.
Uamuzi huo imetolewa leo na Jaji Cyprian Mkeha, baada ya pande zote mbili katika kesi hiyo kuondoa mapingamizi yao ya awali waliyowasilisha mahakamani hapo.
"Kuhusu maombi ya mawakili wa Mdee na wenzake kuwa maombi yenu ya kutaka kuwaita Wadhamini saba wa Chadema na watu watatu walioambatanisha viapo vyao katika kiapo kinzani, ni vizuri mkayawasilisha muda utakapofika na sio saa hizi," amesema Jaji Mkeha.
Kesi hiyo iliitwa kwa ajili ya kutolewa uamuzi wa ombi la mawakili wa Mdee na wenzake la kutaka kuwasilisha mapingamizi ya awali ambapo mahakama iliwakubalia ombi hilo.
Mdee na wenzake 18 walifungua kesi hiyo Julai 21 mwaka huu mahakamani hapo dhidi ya Chadema, Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Tume ya Taifa ya Uchaguzi, wakipinga uamuzi wa Baraza Kuu la Chadema kuwavua uanachama, Mei 11, mwaka 2022.
Awali, wakili wa wabunge hao Ipilinya Paya alieleza mahakama hiyo kuwa anaondoa mapingamizi manne walikuwa wamewasilisha mahakamni hapo dhidi ya kiapo kinzani kilichowasilishwa na wajibu maombi ambao ni Bodi ya Wadhamini iliyosajiliwa na Chadema.
Wakili Paya amedai kuwa amefikia uamuzi huo wa kuondoa mapingamizi hayo ili kuruhusu kesi ya msingi isikilizwe kwa wakati na kutolewa uamuzi.