Mawaziri 22 Afrika kujadili jinsia

Muktasari:

  • Mkutano huu uliaondaliwa na Serikali kwa kushirikiana na Shirika la Umoja wa Mataifa la Wanawake na Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF Afritac East) litawakutanisha mawaziri kutoka nchi 22 barani Afrika.

Dar es Salaam. Tanzania inatarajiwa kuwa mwenyeji wa mkutano wa kimataifa wa mawaziri wanaohusika na fedha na masuala ya jinsia utakaofanyika kuanzia Novemba 15 hadi 17.

 Mkutano huu uliaondaliwa na Serikali kwa kushirikiana na Shirika la Umoja wa Mataifa la Wanawake na Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF Afritac East) litawakutanisha mawaziri kutoka nchi 22 barani Afrika.

Akizungumza leo Novemba 13 kuhusu mkutano huo Waziri wa Fedha, Dk Mwigulu Nchemba amesema utaoa fursa kwa washiriki kujadili namna bora ya kushughulikia athari za mapungufu ya kijinsia katika uchumi jumla.

Mbali na hilo Dk Nchemba amesema mkutano huo utachochea ufadhili wa masuala ya usawa wa kijinsia na uwezeshaji wa wanawake ili kufikia malengo ya maendeleo endelevu.

Waziri Nchemba amebainisha kuwa siku ya kwanza ya mkutano itahusisha mawaziri wenye dhamana ya fedha na wenye dhamana ya jinsi na wanachama wa IMF Africat East.

“Mkutano wa mawaziri utajikita kwenye kuangalia hatua iliyofikiwa kwenye utekelezaji wa ahadi zilizowekwa za majukwaa ya jinsia. Baadhi ya masuala yatakayojadiliwa ni athari za uchumi jumla katika usawa wa kijinsia na jukumu la upangaji wa bajeti unaozingatia jinsia.

“Siku ya pili na ya tatu itakuwa warsha ya kujenga uwezo kwa ajili ya wataalam wa nchi washiriki ambapo itajikita kujenga uelewa wa upangaji bajeti inayozingatia usawa wa kijinsia katika sera za umma,” amesema Dk Nchemba

Kwa upande wake Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dk Dorothy Gwajima alisema kufanyika kwa mkutano huo nchini kunazidi kuongeza sifa kwa Tanzania katika harakati zake za kuweka usawa wa kijinsia.

“Tutakwenda kujadili namna ya kuongeza uwekezaji ili kuzia na kukabiliana na ukatili wa kijinsia, uwekezaji kwenye teknolojia na uvumbuzi unaolenga usawa wa kijinsia, haki na usawa wa kiuchumi. Wataalam watajifunza jinsia ya kuzingatia usawa wa kijinsia kwenye utekelezaji wa miradi, upangaji wa bajeti na mambo mengine mengine yanayohusiana na hayo,” amesema Dk Dorothy.

Mwakilishi Mkazi wa UN Women Hodan Addou alisema huo ni mkutano wa kwanza kufanyika barani Afrika ukiwakutanisha mawaziri hao ambao wana jukumu kubwa la kuhakikisha pengo la jinsia halina nafasi katika uchumi.

Naye Mkurugenzi wa IMF Afritac East, Xiangming LI amesema endapo kutakuwa na juhudi za makusudi za kuondoa pengo la kijinsia kwenye uchumi, wanawake na wasichana wanaweza kuchangia asilimia 80 ya uchumi wa dunia.