Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mazishi dereva wa bodaboda yafanyika usiku chini ya ulinzi Siha

Jeneza lenye mwili wa kijana Emmanuel Mwandry, mkazi wa kijiji cha Ngirinyi, kata ya Nasai ukiwa juu ya gari la Mkuu wa Wilaya ya Siha, mkoani Kilimanjaro. Jeneza hilo linadaiwa kuwekwa kwenye gari hilo na vijana wa bodaboda, Juni 16, 2026.

Muktasari:

  • Tukio hilo lilitokea Juni 16, 2026 baada ya mamia ya madereva bodaboda, Wilaya ya Siha, mkoani Kilimanjaro kuibua vurugu walipokwenda kuchukua mwili wa mwenzao uliokuwa umehifadhiwa katika Hospitali ya KCMC, akidaiwa kufariki kwa kugongwa na gari la polisi katika eneo la Uuwo, Mwika wilaya ya Moshi.

Siha. Wakati mwili wa kijana Emmanuel Mwandry (20) ukizikwa chini ya ulinzi wa polisi saa 2:30 usiku baada ya kuibuka vurugu kwenye mazishi yake juzi, Mkuu wa Wilaya ya Siha, mkoani Kilimanjaro, Dk Christopher Timbuka amesimulia kilichotokea.

Kijana huyo, mkazi wa Ngirinyi, Kata ya Nasai, wilayani Siha, alifariki dunia Juni 12, 2026 kwa madai ya kugongwa na gari katika eneo la Uuwo, Mwika alipokuwa akikimbizwa na Polisi akihisiwa amebeba mirungi, hali iliyosababisha kuibuka kwa purukushani zilizopelekea kifo chake.

Mazishi ya kijana huyo yaliyofanyika juzi usiku,  awali yalikumbwa na vurugu zilizotokana na madai ya Polisi kukamatwa kwa madereva bodaboda mjini Moshi ambao walikuwa kwenye msafara kwenda kuchukua mwili wa kijana huyo katika Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Kaskazini, KCMC.

Vurugu hizo, ambazo zilianza tangu asubuhi wakati mwili wa marehemu ukichukuliwa kutoka Hospitali ya KCMC, zilisababisha ibada ya mazishi kushindwa kufanyika baada ya viongozi wa dini waliokuwa wamefika eneo la mazishi kuondoka kutokana na sintofahamu iliyojitokeza.

Hata hivyo, vijana hao waliendelea na vurugu hizo huku wakichukua jeneza lenye mwili wa kijana huyo na kuliweka juu ya gari la Mkuu wa Wilaya ya Siha, Dk Timbuka, aliyefika msibani hapo, wakishinikiza wenzao waliokamatwa mjini Moshi waachiwe kabla ya shughuli za mazishi kuendelea.

Licha ya kuachiwa kwa wenzao waliokuwa wanashikiliwa mjini Moshi, vurugu ziliendelea wakitoa madai mengine mapya ya kutaka pikipiki ya marehemu iletwe msibani hapo.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka eneo la tukio, ilipofika usiku askari polisi waliokuwa wakisimamia usalama walitumia mabomu ya machozi kuwatawanya vijana waliokuwa wakifanya vurugu, hatua iliyowawezesha polisi kulishusha jeneza lililokuwa juu ya gari la mkuu wa wilaya.

Baada ya jeneza kushushwa, watu 10 walichaguliwa kulibeba hadi makaburini, ambako mwili wa kijana huyo ulizikwa baada ya kufanyika kwa sala fupi ya mazishi bila kuwepo kiongozi yeyote wa dini.

Hata hivyo, wakati wa maziko, eneo hilo lilikuwa chini ya ulinzi wa polisi wenye silaha huku vijana waliokuwa wamesababisha vurugu wakiwa mafichoni.

Mwili wa marehemu ulizikwa usiku giza likiwa limetanda, na waombolezaji wakitumia mwanga wa tochi na taa za simu kuangazia shughuli hiyo ya maziko.

Akizungumza kuhusu tukio hilo, Dk Timbuka amesema baadhi ya vijana waliohusika na vurugu hizo walikuwa wamelewa.

"Vijana hawa walikuwa wamepanga kumsindikiza mwenzao kutoka KCMC hadi Siha. Ukiwaangalia, wengi walioleta tafrani walikuwa wametumia vilevi na hawakuwa katika hali ya kawaida," amesema Dk Timbuka.

Amesema kuwa idadi kubwa ya pikipiki zilizokuwa kwenye msafara huo, iliathiri usafiri katika Barabara Kuu ya Moshi–Arusha kwa muda mrefu, jambo lililosababisha hatua za kuwadhibiti kuchukulia.

"Walipofika Siha walidai hawatazika mpaka wenzao waachiwe. Walipoachiwa, wakaja na madai mengine ya kutaka pikipiki ya marehemu ipatikane. Tuliwaomba wasubiri baada ya mazishi tufuatilie suala hilo, lakini walitaka ipatikane papo hapo. Wakazuia shughuli za mazishi na kulipandisha jeneza kwenye gari la DC," amesema Dk Timbuka.

Dk Timbuka amesema kutokana na hali ya vurugu kuendelea, iliwalazimu kutumia nguvu kuwatawanya.

"Ilibidi tutumie nguvu kidogo ili jeneza lishushwe kwenye gari la DC na shughuli za mazishi ziendelee. Saa moja kuelekea saa mbili usiku ndipo mazishi yalifanyika," amesema.

Amesema kwa sasa hali ya usalama wilayani Siha ni shwari na shughuli zinaendelea kama kawaida.

Naye, Diwani wa Kata ya Nasai, Samson Maseri amesema kutokana na vurugu hizo waombolezaji waliokuwa msibani hapo walikaa hadi usiku wa saa 2:30 baada ya vurugu kutulia ndipo walizika.

“Walifanya vurugu tangu asubuhi wakidai kuwa mwenzao amedhulumiwa uhai wake, lakini kuna wenzao 10 ambao walikuwa wamekamatwa na wakasema bila ya wenzao kuachiliwa hawawezi kuzika. Baadaye waliachiliwa, lakini tukaamini kwamba hali ingetulia, haikuwa hivyo," amesema diwani huyo.