Prime
Mazoea yanavyokwaza utekelezaji wa sheria
Muktasari:
- Licha ya Tanzania kuwa na utajiri wa sheria, kanuni na sera zinazosimamia ujenzi, mifugo na misitu na masuasla mengine mengi, baadhi ya wananchi wanaendelea kufanya shughuli zao kwa mazoea kutokana na ama uelewa mdogo au upuuzaji wa sheria hizo.
Dar es Salaam. Licha ya Tanzania kuwa na sheria, kanuni na sera zinazosimamia karibu kila shughuli ya kijamii na kiuchumi, bado uelewa mdogo wa wananchi au upuuzaji wa masharti hayo umeendelea kuwa chanzo cha migogoro, uharibifu wa mazingira, ujenzi usiofuata utaratibu na matumizi yasiyo sahihi ya rasilimali za taifa.
Wataalamu wa sheria na utawala bora wanasema shughuli za wananchi kuanzia ujenzi wa nyumba, ufugaji wa mifugo, matumizi ya ardhi, ukataji miti hadi uhifadhi wa mazingira, zinaongozwa na sheria mahsusi zinazolenga kulinda usalama wa wananchi, mazingira na maendeleo endelevu.
Hata hivyo, yapo mazoea ya wananchi wengi kufanya shughuli hizo bila kufahamu kuwa zipo sheria zinazobainisha wajibu wao na mipaka ya matumizi ya rasilimali husika, achilia mbali wale wanaozipuuzia.
Wataalamu hao wanasema hali hiyo inaweza kuwaweka watu wengi matatani pale usimamizi wa sheria hizo ukitiliwa mkazi, kwa kuwa kutokujua sheria hakumwondolei mtu wajibu wa anapoikiuka.
Sheria zinazokiukwa na wengi
Moja ya sheria zinazokiukwa kila kukicha, ni Sheria ya Ujenzi Na. 13 ya mwaka 2007 ambayo inaweka masharti ya usalama wa majengo, vibali vya ujenzi na viwango vinavyopaswa kuzingatiwa kabla na wakati wa ujenzi.
Pia, Sheria ya Mipango Miji Na. 8 ya mwaka 2007 inayoelekeza matumizi sahihi ya ardhi mijini kwa kuhakikisha maeneo yanapangwa kulingana na matumizi yaliyokusudiwa.
Kwa upande wa umiliki wa ardhi, Sheria ya Ardhi Na. 4 ya mwaka 1999 pamoja na Sheria ya Ardhi ya Vijiji Na. 5 ya mwaka 1999 zinaweka utaratibu wa umiliki na matumizi ya ardhi nchini.
Katika sekta ya mifugo, Sheria ya Magonjwa ya Wanyama Na. 17 ya mwaka 2003 inayolenga kudhibiti magonjwa ya mifugo na kulinda afya ya wanyama pamoja na Sheria ya Ustawi wa Wanyama Na. 19 ya mwaka 2008 inayoweka wajibu wa kuhakikisha mifugo inatunzwa katika mazingira yanayofaa.
Si hizo tu, ipo Sheria ya Ardhi ya Malisho na Rasilimali za Chakula cha Mifugo Na. 13 ya mwaka 2010 inayosimamia matumizi ya maeneo ya malisho na kusaidia kupunguza migogoro kati ya wafugaji na watumiaji wengine wa ardhi.
Vilevile katika sekta ya misitu, ipo Sheria ya Misitu Na. 14 ya mwaka 2002 pamoja na Sheria ya Usimamizi wa Mazingira Na. 20 ya mwaka 2004 zinazoweka msingi wa uhifadhi wa misitu, matumizi endelevu ya rasilimali na ulinzi wa mazingira.
Mbali na sheria hizo, zipo sera mbalimbali zikiwamo Sera ya Taifa ya Misitu ya mwaka 1998, Sera ya Taifa ya Mifugo ya mwaka 2006 na Sera ya Taifa ya Maendeleo ya Makazi ya mwaka 2000, zinazotoa mwelekeo wa maendeleo ya sekta hizo.
Aidha, serikali za mitaa zimepewa mamlaka ya kutunga sheria ndogo kulingana na mazingira ya maeneo yao ili kudhibiti changamoto kama ujenzi holela, mifugo kuzurura na uharibifu wa mazingira, ambazo si wananchi wengi wanazifahamu wala kuzitekeleza.
Wananchi bado
Licha ya uwepo wa mfumo huo wa kisheria, sera na taratibu, baadhi ya wananchi wanasema hawana uelewa wa kutosha kuhusu taratibu zinazopaswa kufuatwa.
Miongoni mwao ni , Jilili Manyakenda, mfugaji wa Didiya katika Manispaa ya Kahama, Shinyanga anayesema amekuwa akifuga mifugo kwenye maeneo anayoona yanafaa bila kujua kama yametengwa rasmi kwa shughuli hiyo.
"Nimekuwa nikitumia eneo hili kwa sababu kuna malisho ya kutosha. Sijui kama kuna sheria inayobainisha maeneo yanayoruhusiwa kufugia," anasema.
Kwa upande mwingine, Abdallah Selemani mkazi wa Wilaya ya Uyui mkoani Tabora, anayejihusisha na ujenzi wa nyumba za makazi, anasema wananchi wengi hujikita katika umiliki wa kiwanja pekee, bila kufahamu masharti mengine ya ujenzi.
"Mtu akinunua kiwanja huangalia kama ana hati au makubaliano ya umiliki. Kuhusu vibali na masharti mengine ya ujenzi, wengi hatuna uelewa wa kutosha," anasema.
Kauli hizo zinaonyesha namna uelewa mdogo wa sheria unavyoweza kusababisha migogoro, hasara za kifedha na hata hatua za kisheria.
Fursa kujua sheria
Wakali hali halisi iko hivyo, Wakili Hemed Waziri anasema sheria zinazohusu shughuli za wananchi zipo wazi, lakini changamoto kubwa ni wananchi wengi kutopata fursa ya kuzifahamu.
Anasema kabla ya kuanza ujenzi, ni lazima kujiridhisha kuwa matumizi ya eneo yanaendana na aina ya mradi unaotarajiwa.
"Huwezi kujenga kila kitu mahali popote. Lazima ujue eneo limetengwa kwa matumizi ya makazi, biashara, viwanda au shughuli nyingine. Kila eneo lina matumizi yake," anasema.
Anaongeza kuwa maeneo ya hifadhi ya reli, barabara na mito yamewekewa mipaka kwa mujibu wa sheria kwa ajili ya kulinda usalama wa wananchi na miundombinu.
"Huwezi kujenga ndani ya hifadhi ya reli, barabara au mto kwa sababu tu kuna nafasi. Sheria imeweka mipaka ya mita 25.5 kutoka barabarani au relini," anasema.
Kwa mujibu wa Hemed, kila mjenzi anatakiwa kuwa na ramani iliyoidhinishwa na kupata kibali kutoka mamlaka husika kabla ya kuanza ujenzi.
Vivyo hivyo, Wakili Alloyce Komba anasema kutokujua sheria si kinga dhidi ya uwajibikaji, anawataka wananchi kujifunza sheria zinazosimamia shughuli wanazofanya.
Anasema changamoto hiyo inaonekana pia katika sekta za mifugo na misitu ambako baadhi ya wananchi hutumia rasilimali hizo bila kufahamu mipaka iliyowekwa na sheria.
Usimamizi endelevu
Kutokana na ombwe la ufahamu lililopo, Dk Anna Henga wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), anasema changamoto nyingine ni usimamizi usio endelevu wa sheria, hali inayozifanya mamlaka kuchukua hatua baada ya matatizo kujitokeza badala ya kuyazuia mapema.
"Jamii inaweza kuendelea kuishi kwa mazoea kwa sababu inaona hatua zinazochukuliwa ni za muda. Hakuna usimamizi unaoonekana kuwa wa kudumu," anasema mkurugenzi hiyo ambaye pia mwanasheria.
Kauli ya Dk Henga inasisitizwa na Mchambuzi wa siasa na utawala bora, Hamduny Marcel, kuwa hayo yote yanachangiwa na utamaduni wa kusubiri matatizo yatokee ndipo hatua zichukuliwe.
"Ni tatizo la uwajibikaji ambalo limejengeka katika jamii. Watu wengi wamezoea kushughulikia matatizo baada ya kutokea," anasema.
Akizungumzia suluhisho, Marcel anasema utoaji wa elimu ya sheria kwa wananchi na uwajibikaji wa taasisi, ni nguzo muhimu za kujenga jamii inayoheshimu sheria.
Anakubali kwamba uwepo wa sheria, kanuni na sera pekee hauwezi kuondoa changamoto ikiwa wananchi hawazifahamu na mamlaka hazisimamii utekelezaji wake kwa uthabiti.
Hivyo, anasisitiza kuwa sheria za ujenzi, mifugo, misitu na mazingira zimewekwa si kwa lengo la kuzuia maendeleo ya wananchi, bali kuhakikisha shughuli hizo zinafanyika kwa usalama, utaratibu na kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho, hivyo wananchi hawana budi kuzifahamu na kuzifuata.