Mbaroni akidaiwa kujaribu kuua watoto wa kambo kwa sumu

Muktasari:

Mwita anadaiwa kuwa na ugomvi wa muda mrefu na mkewe, ikiwa pamoja na kumpiga mbele ya watoto wao.

Mwanza. Mkazi wa Mtaa wa Igelegele kata ya Mahina wilaya ya Nyamagana, Kichere Mwita (48) anadaiwa kushikiliwa na Jeshi la Polisi mkoani Mwanza kwa tuhuma za kujaribu kuwauwa watoto wa kambo kwa kuwawekea sumu kwenye chakula.

Akizungumza na Mwananchi leo Jumatatu Oktoba 3, mke wa Kichere, Deniza Felesiana (31) amesema mumewe alijaribu kutekeleza tukio hilo kwa kuweka sumu inayodhaniwa kuwa ya panya kwenye chupa iliyokuwa imehifadhi uji kwa ajili ya watoto hao.

"Nina watoto watano lakini watatu ambao ndiyo alitaka kuwadhuru alinikuta nao kabla hatujaoana, wanasoma shule ya msingi Igelegele mmoja ana miaka 13, wa pili 10 na mwingine anasoma darasa la kwanza ana miaka 7," amesema Deniza

Deniza amesema tukio hilo ni mwendelezo wa visa anavyofanyiwa na mumewe, kwani Septemba 28,2022 usiku mumewe huyo alimshushia kipigo huku akiwa utupu mbele ya watoto hao akimtuhumu kutotenga muda wa kuwa naye faragha.

Mwanamke huyo ambaye anajishughulisha kuuza mahindi katika mashine iliyoko eneo hilo anasema analazimika kufanya hivyo ili kupata fedha ili kukidhi mahitaji ya watoto wake watano.


"Siyo kwamba napenda kuchelewa kurudi nyumbani, nalazimika kufanya hii biashara za mahindi hadi usiku kwa sababu mme wangu akiondoka haachi kodi ya meza, sasa nisipo fanya hivi familia yangu itakufa kwa njaa.

"Baba wa hawa watoto watatu anaitwa, Japhet Ernest anaishi Ngara mkoani Kagera. Tulihitilafiana tukaachana baada ya muda nikakutana na huyu (Kichere) akaniahidi kwamba tutashirikiana kuwalea nashangaa anataka kuwadhuru," alisema

Akieleza jinsi alivyogundua kitu anachodai kuwa ni sumu, Deniza anasema siku ya tukio alimuona mmewe akiwa ameinama kwenye chupa ya uji iliyokuwa chumbani na kushindwa kumtilia shaka, kwani aliamini anafanya maandalizi ya kwenda kazini.


"Alikuwa ana tabia ya kuchukua hela zangu za mahindi lakini aliponiona nimeingia chumbani alinyanyuka na kuchukua viatu vyake akavaa kisha akaaga kwamba anaenda kazini," anasema

Anasema baada ya mmewe kuondoka, ilipofika Saa 9 alasiri watoto hao waliporejea kutoka shuleni alichukua chupa hiyo kwa ajili ya kumimina uji kwenye kikombe ndipo alipobaini chakula hicho kinatoa harufu isiyo ya kawaida.

"Baada ya kunusa harufu ya ajabu nilimpelekea jirani yangu akasema ni harufu ya sumu ya kuulia panya. Nilivyoambiwa vile nilichukua ile chupa nikaumwaga nje, lakini uji wa kwenye kikombe na ile chupa tulivipeleka kwenye uongozi wa mtaa," anaeleza Deniza.

Anaongeza; "Baada ya kubaini kuwa kulikuwa na sumu majirani zangu walirudi na kuweka mtego kusha kumkamata tukampelekea kituo cha Polisi Nyakato ambako anashikiliwa hadi leo wakati uchunguzi ukiendelea."

Baadhi ya majirani akiwamo Ndaki Mathias, anasema amekuwa akishuhudia wanandoa hao wakiwa kwenye ugomvi kila mara jambo ambalo limekuwa likizua taharuki kwa wakazi wa eneo hilo.

Pia, alisema mbali na ugomvi, mwanaume huyo amekuwa akimdhalilisha mkewe kwa kumpiga hadharani akiwa utupu hata mbele ya watoto wao.

"Hadi kuchukua hatua ya kumkamata na kumpeleka kituo cha Polisi ni kwa sababu tumechoshwa na ukatili wake. Tuliona tusipochukua hatua madhara makubwa yanaweza kujitokeza," alisema Mathias

Naye, Veronica Josephat aliiomba serikali kuingilia kati suala hilo ili kuinusuru familia hiyo kabla haijapata madhara zaidi.

Naye Mjumbe wa Serikali ya Mtaa wa Igelegele kata ya Mahina mkoani hapa, Charles George alikiri kupokea malalamiko ya mwanamke huyo kushushiwa kipigo na mmewe.

Kuhusu tukio la mwanaume huyo kuweka sumu kwenye chakula, alikiri kutokea tukio hilo na kusema baada ya kubaini kubaini uwepo wa sumu alichukua kikombe chenye uji huo na kukikabidhi kwa maofisa wa polisi wa Kituo cha Polisi Nyakato.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Mtaa huo, Gerald Pondi aliitaka jamii kutofumbia macho vitendo vya ukatili kwa kutoa taarifa katika madawati ya jinsia na Mamlaka ya Serikali ya Mtaa kabla hawajapata madhara.

Hata hivyo, alipopigiwa simu leo, Kamanda wa Polisi mkoa wa Mwanza, Ramadhani Ng'anzi bila kusema iwapo wanamshikilia mwanaume huyo, amesema taarifa za kuwepo tukio hilo hazijafika ofisini kwake kuahidi kutoa taarifa litakapofika ofisini kwake.

"Sina taarifa kama limeripiwa hilo tukio labda ngoja nilofatilie nitatoa taarifa," alisema Ng'anzi