Mbaroni akituhumiwa kubaka, kulawiti watoto 15 Iringa

Kamanda wa Polisi mkoani Iringa, Allan Bukumbi

Muktasari:

  • Wakati dunia ikiadhimisha siku 16 za kupiga ukatili wa kijinsia, Dereva Bajaji wa Manispaa ya Iringa, Alex Msigwa (34) anashikiliwa na polisi kwa tuhuma za kuwabaka, kuwalawiti watoto 15 kwa nyakati tofauti mkoani Iringa.

Iringa. Jeshi la Polisi mkoanj Iringa limemtia mbaroni dereva bajaj, Alex Msigwa (34), akituhumiwa kubaka na kulawiti watoto 15 katika maeneo tofauti ya Manispaa ya Iringa.

Alex ametiwa mbaroni wakati Dunia ikiadhimisha siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia ikiwamo ubakaji na ulawiti kwa watoto.

Kwa siku za hivi karibuni kumekuwa na matukio ya ukatili kwa watoto katika mkoani Iringa hasa ndani ya Manispaa ikiwamo ubakaji, ulawiti, mauaji na vipigo huku imani za kishirikina zikitajwa kuwa sababu.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa, ACP Allan Bukumbi inaeleza mtuhumiwa huyo alikuwa akijifanya ofisa ustawi wa jamii na wakati mwingine askari polisi ili iwe rahisi kutekeleza adhma yake.

Amesema alikuwa akiwakamata watoto wanaozurura na kutembea usiku kisha kuwafanyia ukatili huo.

"Alikuwa anawatishia kwa kisu watoto wenye umri kati ya miaka sita hadi 12 na wakati mwingine akiwapatia fedha," amesema Bukumbi

Mmoja wa wazazi wenye watoto hao (jina limehifadhiwa) ameiambia Mwananchi Digital leo Alhamisi Disemba 7, 2023 kuwa alipopata taarifa za mwanae kulawitiwa aliamua kumkagua na kugundua kuwa amebakwa na kulawitiwa.

"Sikuamini kabisa nilipoambiwa lakini baada ya kumkagua nikagundua ameingiliwa, nilikuja polisi moja kwa moja nilipofika kituoni nikaanguka chini, nashukuru mtuhumiwa amekamatwa," amesema

Mzazi mwingine ambaye watoto wake wawili wanadaiwa kufanyiwa ukatili huo, amesema tangu saa moja hadi saa saba usiku aliwatafuta watoto wake bila mafanikio.

"Saa saba usiku ndio nikawakuta, wa kike alikuwa amebakwa vibaya na kulawitiwa. Kitendo kiliniumiza sana, nilikuja Hospitali ndio nikaambiwa niende kituo cha polisi," amesema mama huyo.

Mzazi mwingine amesema mtuhumiwa aliwaita watoto akijitambulisha kwa jina la afande Jack, aliwatishia watoto wanne kuwa atawapeleka kituoni kwa sababu wanacheza mpaka usiku, alifika nao mitaa wa kwa mduda akawaambia wadogo warudi akabaki na wakubwa," amesema na kuongeza;

"Tuliwatafuta watoto hadi saa nne usiku na walikuwa wamelawitiwa vibaya."

Wakizungumza na Mwananchi kwa nyakati tofauti baadhi ya wakati wa Manispaa ya Iringa wamesema ulevi, imani za kishirikina na tamaa ndizo chanzo Cha matukio hayo.

"Watoto 15, mtu anatuhumiwa kuwafanyia ukatili kama sio ushirikina ni nini? Hali hii ni hatari ikiachwa iendelee," amesema Judith Mgeni, mkazi wa Kihesa Manispaa ya Iringa.

Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Halima Dendego amekemea matukio hayo akiagiza vyombo vya ulinzi kutowafumbia macho wote watakaokamatwa na kubainika kufanya vitendo hivyo.

"Ifike mahali tuseme basi, inatosha matukio haya ya kinyama, tunafanya ukatili huu ili tupate nini? Hivi unaendaje kwaa katoto, iwaje? Nimeviagiza vyombo vya ulinzi na usalama kushughulikia suala hili," amesema Dendego.