Mbaroni kwa tuhuma za kumlawiti mtoto Dar

Muktasari:

  • Wakati takwimu zikionesha ongezeko la vitendo vya ukatili wa kingono kwa watoto, Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam inashikilia kijana mmoja kwa tuhuma hizo.

Dar es Salaam. Jeshi la polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam limethibitisha kumshikilia mtu mmoja aliyetajwa kwa jina la Marwa anayedaiwa kumfanyia ukatili wa kingono mtoto mmoja ambaye ni mwanafunzi wa shule ya Msingi Global iliyopo Wilaya ya Kinondoni.

Awali Hospitali ya Kimkoa Mwananyamala ilithibitisha kupokea wanafunzi nane kutoka shule hiyo waliokuwa wanadaiwa kufanyiwa vitendo hivyo.Akizungumza Dar es Salaam leo Mei 26/2022 Kamanda wa Polisi wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro amesema baada ya kufanyika uchunguzi wamebaini mtoto mmoja amefanyiwa vitendo hivyo vya unyanyasaji wa kingono.

“Kweli watoto wanane walipelekwa hospitali lakini ilikuwa paniki na hasira  kilichodhihirika ni mtu mmoja aliyefanyiwa vitendo hivi vya unyanyasaji wa kingono,”amesema Kamanda MuliroAmesema hata hivyo mtuhumiwa huyo bado wanaendelea kumshikilia mahabusu katika kituo kikuu cha Polisi Osterbay wakati akisubiri mifumo ya sheria ifanye kazi yake kwa kufikishwa Mahakamani.

Mwananchi ilifika katika eneo la shule hiyo ili kuzungumza na Mwalimu Mkuu wa shule hiyo ambaye kwa wakati huo hakuwepo ofisini kwake huku walimu wengine wakigoma kutoa ushirikiano.

Tukio jingine la kikatiliWakati hayo yakiendelea limeripotiwa na msamalia mwema tukio la mtoto mwenye umri wa miaka nane kupigwa na baba yake usiku kucha baada ya kugundua mtoto huyo amekuwa akifanyiwa vitendo vya ulawiti.

Msamaria huyo ambaye hakutaka kutajwa jina lake amesema baba huyo amekuwa na kawaida ya kumpiga mtoto huyo."

Jana usiku pia alirudia tena tabia yake ya kumpiga ndipo mimi pamoja na majirani wengine tulitoka kwenda kumuokoa mtoto huyo katika kipigo hicho na katika kumuhoji sababu ya kufanya hivyo ndipo alipoeleza kuwa amegundua kuwa mtoto anafanyiwa vitendo vya ukatili wa kingono,"amesema.

Amesema baada ya hapo walichukua hatua mbalimbali ikiwepo kumpeleka baba huyo kituo cha polisi, kumfikisha mtoto katika kituo cha afya pamoja na kutoa taarifa katika uongozi wa mtaa.

Mama wa mtoto huyo amesema aligundua kuwa mtoto wake amekuwa akifanyiwa vitendo hivyo vya ukatili baada ya kuona baadhi ya mabadiliko kwa mtoto wake ambayo yalimpa shaka na kuamua kumkagua ndipo alipogundua kuwa amefanyiwa vitendo hivyoAlitoa wito kwa wazazi wengine pamoja na kufanya kazi za kujizalishia kipato pia wajitahidi katika kuwachunguza na kuwa karibu na watoto wao na kuzungumza nao ili waweze kugundua yanayowasibu.

"Watoto wetu wako katika hatari ya kufanyiwa vitendo vya ukatili haswa kwa nyakati hizi, wazazi inapaswa tuwajibike katika kuwalinda watoto wetu,"amesema.

Amesema kutumia kwake muda mwingi katika kutafuta rizki kuliko anaamini kumechangia kwa namna moja au nyingine kumepelekea kutokea kwa jambo hiloNaye Mtendaji wa mtaa huo, (jina tunalihifadhi)  amesema majira ya asubuhi alipokea taarifa ya mtoto kupigwa kutoka kwa mmoja wa wakazi wa eneo hilo hivyo aliamua kuchua hatua mbalimbali ikiwemo kufika katika eneo la tukio na kuahirikiana kumkamata baba huyo na kumripoti polisi.

Alisema kwa taarifa alizozipata mtoto huyo alianza kufanyiwa vitendo vya ukatili katika eneo walilokuwa wakiishi awaliKwa upande wake,Waziri wa Maendeleo ya Jamii Jinsia Wanawake na Makundi Maalumu, Dk Dorothy Gwajima amesema kulingana na matukio yanayoendelea kujitokeza ya vitendo vya kikatili kwa watoto amebaini wazazi wengi hawana muda wa kukaa na watoto wao.

“Mtoto anarudi kutoka shule anafika nyumbani anajikuta yuko peke yake wazazi wote wapo kwenye mihangaiko ya uchumi hivyo wanakosa muda wa kumkagua mtoto na kuongea naye,”amesema.

Dk GwajimaPia Dk Gwajima amebaini kuwa kamati ya ulinzi ya wanawake na watoto kwenye maeneo husika zinatakiwa kuwa imara sambamba na miongozo yake ili ziweze kushirikiana na wazazi katika suala zima la malezi.