Mbaroni kwa tuhuma za kumuua mama yake mzazi

Muktasari:

  • Mkazi wa Wilaya ya Hanang' Mkoani Manyara anashikiliwa na polisi akituhumiwa kumuua mama yake mzazi ambaye ni mwalimu mkuu wa shule ya msingi Arkisi baada ya kumuomba fedha na kumnyima.

Hanang'. Mwalimu mkuu wa Shule ya Msingi Arkisi Wilayani Hanang’ Mkoani Manyara, Kasi Salai (50) ameuawa na mtoto wake wa kumzaa John Ammi (20) baada ya kuombwa fedha za matumizi na kisha akamnyima.


Kamanda wa polisi wa mkoa wa Manyara, Kamishna Msaidizi (ACP), Marrison Mwakyoma, akizungumza na Mwananchi digital leo Agosti 2, amesema tukio hilo limetokea jana Agosti mosi.


Kamanda Mwakyoma amesema chanzo cha tukio hilo ni mwalimu huyo kuombwa fedha na mtoto wake wa kumzaa ili afanye matumizi yake, akamnyima kisha akamuua.


Amesema kijana huyo baada ya kumuomba mama yake fedha za matumizi na mama yake kumwambia hana chochote alichukia.
“Baada ya mtoto huyo kunyimwa fedha na mama yake alimpiga kichwani na kitu butu kisha mwalimu huyo akafariki dunia papo hapo,” amesema Kamanda Mwakyoma.


Amesema polisi wanamshikilia mtuhumiwa huyo kwa uchunguzi zaidi kabla ya kumfikisha mahakamani kujibu mashtaka hayo ya mauaji ya mama yake mzazi.


Ametoa wito kwa wananchi wa mkoa huo kutojichukulia sheria mkononi na pindi kukitokea tatizo laa kifamilia ni vyema kusuluhisha kuliko kusababisha mauaji kwani siyo suluhisho.