Mbaroni kwa tuhuma za kumuua mwanaye wa miaka sita

Muktasari:

  • Jeshi la Polisi Mkoani Singida, linamshikilia John Musoma (30) Mkazi wa Kijiji cha Nkonko wilaya ya Manyoni kwa tuhuma kumuua mwanawe mwenye umri wa miaka sita, kwa kumpinga kichwani kwa fimbo.

Manyoni. Jeshi la Polisi Mkoani Singida, linamshikilia John Musoma (30) Mkazi wa Kijiji cha Nkonko wilaya ya Manyoni kwa tuhuma kumuua mwanaye mwenye umri wa miaka sita, kwa kumpinga kichwani kwa fimbo.

Kamanda wa Polisi mkoani wa Singida Stella Mutabihirwa amemtaja marehemu ni James Musoma ambaye aliuawa Mei 4, 2023.

Chanzo cha mauaji hayo kimetajwa ni mtoto huyo kuchelewa kufika shambani alikotakiwa kulinda mtama usiliwe na ndege waharibifu.

Kamanda amesema mbali na mtoto huyo aliyepoteza maisha, kaka yake Joseph Musoma (8) alishambuliwa na baba yao pia na kupata maumivu sehemu mbalimbali za mwili wake.

“Suala la mauaji kwa wilaya ya Manyoni bado ni mtihani mgumu, tunaendelea kutoa elimu kila wakati lakini naona bado limeota mizizi, lakini tutaendelea kutoa elimu na kuwakamata wote wanaojihusisha na matendo hayo ya uvunjifu wa amani,” amesema Stella.

Askofu Mstaafu Kanisa la Pentekoste (FPCT) Singida mjini kati, Dk Paul Samweli, amesema Manyoni inahitaji maombi ya nguvu na pia kutafuta kiini cha mauaji ya binadamu iwe ya bahati mbaya au ya kukusudia.

“Kwa nini nguvu hii ya mauaji inataka kushinda nguvu ya wazazi, dini hata serikali yenyewe, tunatakiwa  kwa pamoja viongozi wa madhehebu ya dini, wazazi na serikali, tukae ili kujua mizizi ya vitendo hivi vibaya kisha tuvipatie ufumbuzi wa kudumu,” amesema Dk Paul.

Katibu wa BAKWATA mkoa wa Singida, Alhaj Burhani Mlau, amesema kitendo cha mzazi kumuua mtoto wake mwenye umri mdogo wa miaka sita, hakivumiliki kwani inaonyesha alitoa adhabu ambayo imepitiliza.

Alhaj Mlau amesema umri ya miaka sita bado mtu hawezi kuwa amejitambua bado anahitaji kusaidiwa kujifunza mambo mengi, ikiwemo kufukuza ndege shambani kwa maelekezo siyo nguvu kubwa kama iliyotumika.