Mbaroni Njombe wakituhumiwa kuchakachua mbolea ya ruzuku

Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Anthony Mtaka

Muktasari:

  • Wakati Polisi mkoani Njombe wakiwakamata watu 10 kwa tuhuma za kuwauzia wakulima mbolea feki kisha, Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA), imemfutia leseni mfanyabiashara mmoja wa mbolea kwa tuhuma hizo.

Njombe. Jeshi la Polisi mkoani Njombe linawashikilia watu 10 kwa tuhuma za kufungasha mbolea feki kisha kuwauzia wakulima mkoani humo.
Wakati watuhumiwa hao wakikamatwa, Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA), imemfutia leseni mfanyabiashara wa mbolea mkoani hapa.
Hayo yamesemwa leo Januari 20, 2023 na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Njombe, Hamisi Issah wakati akizungumza na waandishi wa habari.
Amesema watuhumiwa hao wanaohusika na kusafirisha vyombo vilivyokuwa vikitumika kuchakachua mbolea hiyo na kuwauzia wakulima ikiwemo majenereta
"Kuna watu zaidi ya 10 wamekamatwa na hii inahusisha watu ambao wenye vyombo ambavyo vimesafirisha na watu ambao kwa namna moja au nyingine walihusika kubeba jenereta na mambo mengine," amesema Kamanda Issah.
Pia amesema jeshi hilo linaendelea kufanya uchunguzi kama ilivyo kawaida ili wahusika watakapopatikana wapelekwe mahakamani na sheria iweze kufuata mkondo wake.  
Amewashukuru viongozi wote akiwemo Mkuu wa Mkoa, Mkurugenzi Mtendaji wa udhibibiti wa mbolea wa TFRA na wananchi kwa kutoa ushirikiano uliosababisha kukamata vitu vinavyohusika na uhalifu huo.
Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Anthony Mtaka alitoa wito kwa wafanyabiashara na mawakala wa mbolea mkoani humo wajue Serikali inafuatilia kwa ukaribu suala la mbolea, kwa sababu Rais Samia Suluhu Hassan ametoa fedha nyingi kwa ajili ya kubeba dhamana ya ruzuku ya mbolea ya wakulima.
Amesema sasa inapotokea mfanyabiashara anaingia kwenye tamaa na amepewa leseni na mamlaka za Serikali na kufika mahala kukodisha nyumba , majenereta na kununua mashine ili kutengeneza mbolea feki na kupeleka kwa wakulima ni kufedhehesha Serikali.
"Wananchi wanatukana Serikali kwamba kuna mbolea ya ruzuku kumbe feki, tunalishukuru na kulipongeza jeshi la polisi kwa kuiheshimisha Serikali na tunaomba moyo huu wa askari wetu na vyombo vyetu vyote vya ulinzi na usalama uendelee ili tuweze kuwasaidia wananchi," amesema Mtaka.
Katika hatua nyingine, Mkurugenzi Mtendaji wa TFRA, Dk Stephan Ngailo amesema mamlaka hiyo imemfutia leseni mfanyabiashara mmoja mkoani Njombe anayedaiwa kuchakachua mbolea na kuwauzia wakulima kinyume na utaratibu.
Hata hivyo, Ngailo hakuwa tayari kumtaja mfanyabiashara huyo wala kampuni akisema itaharibu upelelezi.
Amesema pamoja na kumfutia leseni mfanyabiashara huyo ameomba vyombo vingine viweze kuchukua sheria ili kufikishwa mahali panapo stahili na kutakiwa kuwafidia wakulima wote ambao wameweza kuathirika kwa tabia na vitendo hivyo.
Vilevile Ngailo amesema lililofanyika mkoani Njombe chini ya usimamizi wa Mkuu wa Mkoa Anthony Mtaka lifanyike katika mikoa mingine yote nchini hasa mikoa ya Nyanda za Juu Kusini na Mkoa wa Kigoma ili kubaini tatizo kama ambalo limejitokeza mkoani hapa.
"Nawashukuru Mkuu wa Mkoa na timu yako kwa kuweza kufanikisha zoezi hili kukamatwa kwa huyu ambaye alikuwa anafanya ubadhilifu, udanganyifu na uhujumu uchumi ni wazi kuwa hana nia njema na wakulima, wizara yetu ya kilimo na Serikali," amesema Dk Ngailo.