Mbowe amchambua Lowassa

Muktasari:

Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe amesema kiongozi yoyote ndani ya chama hicho anayedhani kuondoka kwake na kujiunga na vyama vingine akiwamo Edward Lowassa ni mwisho wa chama hicho kikuu cha upinzani nchini ni ndoto

Singida. Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe amesema kiongozi yoyote ndani ya chama hicho anayedhani kuondoka kwake na kujiunga na vyama vingine akiwamo Edward Lowassa ni mwisho wa chama hicho kikuu cha upinzani nchini ni ndoto.

Amesema Lowassa aliyejiunga na Chadema Julai 28 mwaka 2015 na kupitishwa kuwa mgombea urais wa chama hicho akiungwa mkono na vyama rafiki vya Ukawa alishindwa kuhimili mikiki mikiki za upinzani na kuamua kurejea CCM, Machi 1.

Mbowe ambaye pia ni Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni alitoa kauli hiyo juzi wakati akizungumza kwenye kikao cha ndani cha wajumbe wa mkutano mkuu wa jimbo la Singida Kaskazini.

“Chadema sio chama cha mtu, hiki ni chama taasisi, yoyote anaweza kuondoka ndani ya Chadema, ataondoka peke yake akiweza sana ataondoka na mke wake.”

“Na ndio sababu kiongozi yoyote aliyejiaminisha akitoka Chadema chama kitakufa, hiki chama hakiwezi kufa,” alisema Mbowe huku akishangiliwa na wajumbe wa mkutano huo

Mbowe alisema, “hata alipokuja Lowassa, tulimhifadhi, tukanuia pamoja lakini pengine hakujua mziki uliokuwa ndani ya upinzani, dhoruba za miaka mwili tu mzee alilegea kuliko mlenda.”

“Tikamwambia mzee wewe kama mgombea wa urais toa kauli, watu wanapigwa risasi, simama kama kiongozi laani. Lowassa wewe ni mgombea urais, watu wamekuunga mkono nchi nzima, umezuiwa kwenda kuwashukuru watu milioni sita, simama lalamika,” aliongeza

Alisema licha ya kumtaka Lowassa ambaye ni waziri mkuu wa zamani kutoa kauli hakufanya hivyo na wakati wote waliwasihi viongozi wanzake wa Chadema kutulia na , “ikafika mahali mzee akaona huku ni balaa, misuko suko, mali zikapotea.”

Mbowe alisema kuna siku Lowassa  alikwenda katika futari (Juni mwaka 2017) akatoa kauli kuhusu masheikh waliowekwa kizuizini, “katika ile futari akatoa neno kuwa Serikali ifike mahali iachie hawa masheikh na kama wana makosa washtakiwe.”

Alisema kauli hiyo ilimfanya kuitwa Makao Makuu ya Polisi wito ambao aliuitikia Juni 27 mwaka 2017 lakini Mbowe ana mnukuu Lowassa akisema, “Kesho yake (baada ya kauli ya Lowassa kuhusu masheikh) ikatoka katika vyombo vya habari, polisi wakamtafuta, mzee saa 11 ananipigia simu, nikwamwambia sisi mbona tunaitwa sana na tangu siku hiyo mzee hakuongea tena na ikafika wakati akaondoka.”

“Lakini (Lowassa) alikuja Chadema na alikuja na watu, lakini alivyoondoka ameondoka na mkewe na watoto wake wawili kwa sababu tumejenga chama taasisi,” alisema

Lowassa alitoa kauli hiyo Juni mwaka 2017, nyumbani kwa aliyekuwa Mbunge wa Ukonga (Chadema), Mwita Waitara (hata hivyo sasa Waitara yuko CCM) ambapo inadaiwa alitoa kauli inayoelezwa kuwa ni ya kichochezi kuhusu kumtaka Rais John Magufuli kuwaachia Masheikh wa Uamusho kuwaachia huru.

Mwananchi lilimtafuta Lowassa kwa simu yake ya kiganjani bila mafanikio ili azungumzie hoja za mwenyekiti huyo wa Chadema kuwa amerejea CCM baada ya kushindwa kuhimili mikiki ya upinzani na si kuwa karudi nyumbani tu kama alivyotamka.

Mbowe na viongozi mbalimbali wa Chadema juzi na jana waligawana majimbo kumi ya Mkoa wa Singida katika ziara ya kujenga chama. Viongozi ha  leo na kesho watakuwa majimbo ya Dodoma kisha watahamia Morogoro.