Mbowe ampa Lema kibarua Katiba Mpya

Muktasari:

Mwenyekiti wa Chadema Taifa, Freeman Mbowe amempa kazi mjumbe wa Taifa wa chama hicho, Godbless Lema juu ya kuanzisha upya harakati za kudai katiba mpya kwa upande wa mikoa ya Kanda ya kaskazini.


Arusha. Mwenyekiti wa Chadema Taifa, Freeman Mbowe amempa kazi mjumbe wa Taifa wa chama hicho, Godbless Lema juu ya kuanzisha upya harakati za kudai katiba mpya kwa upande wa mikoa ya Kanda ya kaskazini.

Mbowe amempa kibarua hicho Lema Leo Machi 1, 2023 katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika Viwanja vya Relini ikiwa ni mapokezi ya kumkaribisha nchini baada ya kukimbia na kwenda kuishi nchini Canada baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020.

Akizungumza katika mkutano huo, mwenyekiti Mbowe amesema kuwa mkutano wa maridhiano waliokaa na Rais Samia Suluhu Hassan hauwezi kuwarudisha nyuma katika harakati zao za kudai katiba mpya.

"Ule mkutano wa maridhiano usiwape Shaka kwamba unaweza kuturudisha nyuma, ni kwamba sauti za wananchi zitaendelea kusikika za kudai haki itakayopatikana kwenye katiba mpya," amesema Mbowe na kuendelea...

"Sasa Lema leo umekuja nakupa kazi ya kuhakikisha harakati hizi zinafanyika vema katika mikoa ya Kanda ya Kaskazini na naamini kazi hii utaifanya vizuri maana mke na watoto umewaacha Canada hivyo nafasi unayo," amesema.


Kwa upande wake Lema aliyewahi pia kuwa Mbunge wa Jimbo la Arusha Mjini, amesema kuwa kazi hiyo ataifanya ingawa siyo kazi rahisi.

"Laiti ningekuwa na uwezo, ningeomba kikombe hiki kiniepuke lakini kwa sababu sina uwezo makamanda tuingie kazini tufanye kazi hii," amesema.

Kwa upande wake mgeni wa heshima, mwanasiasa, Profesa George Wajackoah akizungumza katika mkutano huo amewataka Watanzania watakapoandika Katiba Mpya iwe nzuri yenye kuwafaa kwa matumizi hata vizazi vijavyo.


"Mnapokwenda kuandika Katiba Mpya hakikisheni mnaandika mambo yanayowafaa leo hata kesho kwa watoto wenu kwa utendaji wa haki na uhuru isiwe mbovu Kama ya Kenya," amesema.