Mbowe awachongea wagombea wa CCM

Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe

Muktasari:

Uchaguzi huo unafanyika Novemba 26

Rungwe. Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe amewataka wananchi wanapowasikiliza watawala katika mikutano ya kampeni kutumia nafasi hiyo kuhoji ahadi zilizotolewa katika kampeni za Uchgauzi Mkuu wa mwaka 2015.

Alisema wananchi wasitumie mikutano hiyo kama eneo la starehe na kupita, badala yake waitumie kutafakari mustakabali wa Taifa na utendaji wa waliowachagua ikiwamo wa kutoka chama tawala, ambao kwa kiwango kikubwa wanapaswa kuhojiwa kuhusu ahadi walizotoa.

Mbowe alisema hayo alipokuwa akimnadi mgombea udiwani wa Ibhigi, Wilaya ya Rungwe mkoani Mbeya, Emmanuel Simba.

Mbowe ambaye pia ni mbunge wa Hai, alisema kwa sababu kuna katazo la mikutano ya kisiasa nchini, hawana budi kutumia nafasi ya kampeni hizo kujua mambo mbalimbali waliyoahidiwa ikiwamo ahadi ya kutolewa Sh50 milioni kila kijiji.

Alisema kuna haja ya kubadili mtizamo badala ya kutumia mikutano kama eneo la starehe na mbwembwe, waitumie kutafakari kilichofanyika tangu kumalizika uchaguzi mkuu.

“Jamani vitu vingi vinavyofanyika sasa ni vilivyoahidiwa kwenye awamu iliyopita, ahadi za mwaka 2015 hazijatekelezwa, badala yake nyingine zinakataliwa,” alisema Mbowe.

Alifafanua kuwa kwenye siasa hakuna rafiki wa kudumu wala adui wa kudumu, hivyo utekelezaji wa ahadi ndiyo utapambanua kwa wakati huo rafiki na adui ni nani.

Mbowe ambaye ni kiongozi wa kambi ya upinzani rasmi bungeni, alisema wakati umefika kwa wananchi kutumia masanduku ya kura kuonyesha hasira zao.

Meya kubana viongozi

Akizungumza kwenye mkutano huo, meya wa Jiji la Mbeya, David Mwashilindi alisema ataongeza usimamizi kuhakikisha kila kiongozi wa Chadema anatekeleza majukumu yake kulingana na ahadi zake kwa wananchi.

“Huu siyo wakati wa kubweteka, ni wakati wa kuongeza nguvu kujenga chama,” alisema.

Mwashilindi alisema wananchi wanatambua Chadema ni mkombozi na wao wanalionyesha hilo kwa vitendo.

Aliwataka wananchi kutoruhusu kunyimwa sauti kwenye uamuzi wa masuala yanayowahusu, hivyo wachague mgombea wa Chadema.