Mbunge ahoji fidia ya miaka 10

Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dk Stergomena Tax

Muktasari:

  • Mbunge wa Viti Maalum (CCM), Hawa Mwaifunga amehoji ni lini Serikali itawalipa fidia wananchi wa Kijiji cha Usulo, Kata ya Mbungani, Manispaa ya Tabora baada ya maeneo yao kuchukuliwa na Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ).

  

Dodoma. Mbunge wa Viti Maalum (CCM), Hawa Mwaifunga amehoji ni lini Serikali itawalipa fidia wananchi wa Kijiji cha Usulo, Kata ya Mbungani, Manispaa ya Tabora baada ya maeneo yao kuchukuliwa na Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ).

Mwaifunga ameeleza kuwa maeneo hayo yaliyochukuliwa yamefanyiwa tathimini miaka 10 iliyopita.

Akijibu swali hilo leo Jumatano Aprili 20, 2022 Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dk Stergomena Tax amesema fedha kwa ajili ya fidia zimejumuishwa katika bajeti ya wizara hiyo 2021/22 na wananchi hao wanatarajiwa kulipwa hivi karibuni.

 “Manispaa ya Tabora imefanya tathimini na wamewasilisha wizarani Septemba 2021.  Wizara imekwishawasilisha vitabu hivyo kwa Wizara ya Fedha na Mipango (Hazina) kwa ajili ya uhakiki na malipo, ambapo uhakiki ulikamilika Disemba mwaka 2021,”amesema.

Amesema fedha kwa ajili ya fidia zimejumuishwa katika bajeti ya Wizara ya mwaka 2021/22, inatarajiwa kuwa wananchi husika watalipwa fedha hivi karibuni, mara baada ya wizara kupokea fedha kutoka Wizara ya Fedha na Mipango.

Katika swali lake la msingi, Mbunge wa Viti Maalum (CCM) Hawa Mchafu amehoji ni lini itatatua mgogoro wa ardhi kati ya Jeshi hilo na wananchi kata ya Kiluvya wilayani Kisarawe mkoani Pwani.

Akijibu swali hilo Tax amesema kuwa wanampango wa kusuluhisha migogoro ya ardhi wa miaka mitatu ambapo maeneo 152 nchini yanahusishwa.

Amesema tayari wameshapima maeneo 86 na kufanyia uthamini maeneo 13 huku maeneo 66 upimaji ukiendelea.