Mbunge aitaka Serikali kuchukua hatua uchakachuaji wa mbolea

Mbunge wa Sumbawanga Mjini,  Aeshi Hilaly akizungumza kwenye mkutano wa hadhara  uliofanyika leo Jumatatu Julai 24, 2023 katika Kijiji cha Mponda Kata ya Majengo.

Muktasari:

  • Mbunge wa Sumbawanga Mjini, Aeshi Hillary ametoa rai hiyo baada ya wananchi wa kijiji cha Mponda mkoani Rukwa kulalamika kwamba wananunua mbolea zilizochakachuliwa, jambo linaloathiri kilimo chao.

Rukwa. Mbunge wa jimbo la Sumbawanga Mjini, Aeshi Hilaly ameitaka Serikali kuwachukulia hatua za kisheria baadhi ya wafanyabiashara wanaochakachua mbolea ya ruzuku inayotolewa na Serikali kwa wakulima.

 Hilaly amebainisha hayo leo Julai 24, 2023 wakati akizungumza kwenye mkutano wa hadhara na wananchi wa kijiji cha Mponda kilichopo katika kata ya Majengo mjini Sumbawanga.

Amesema ni vema Serikali ikachukua hatua za kisheria dhidi ya wafanyabiashara wasio na uzalendo wanaolalamikiwa kuchakachua mbolea ambayo hutumika kwenye uzalishaji wa mazao ya kilimo.

“Kila ninapokwenda, kilio ni cha wakulima ni kuhusu kuchakachuliwa kwa mbolea, hali inayofanya uzalishaji wa mazao hususani mahindi kutokuwa mzuri…hawa watu hawana uzalendo hata kidogo, niiombe Serikali ichukue hatua za kisheria kudhibiti kero hiyo,” amesisitiza Hilaly.

Mbunge huyo ameeleza hayo baada ya mmoja wa wananchi wa kijiji cha Mponda, Mwanandenje Siame kutoa malalamiko yake kwa mbunge huyo kwamba mbolea ya ruzuku inayotolewa na Serikali kupitia kwa mawakala inachakachuliwa, jambo linaloathiri uzalishaji wa mazao.

Kwa upande wake, Meneja wa Kanda ya Nyanda za Juu Kusini wa Kampuni ya ETG inayojishughulisha na usambazaji wa pembejeo za kilimo, Hassan Macho amesema kinacholalamikiwa na wakulima kinaweza kuwa na ukweli kwa kuwa malalamiko ya aina hiyo amekuwa akiyasikia kupitia vyombo vya habari.

“Unajua katika shughuli yoyote huwezi kukosa watu wasio waaminifu, hivyo yawezekana na huku kwenye pembejeo za kilimo wapo watu wa aina hiyo, lakini kwenye kampuni yetu hatujawahi kupokea malalamiko ya aina hiyo. Nawashauri wakulima watoe taarifa kama wamekutana na kadhia hiyo kwa kuwa mfumo wa upatikanaji wa mbolea kwa sasa uko wazi.

“Mfumo unajieleza ulinunua kwa nani na kwa utaratibu upi. Wajitokeze na kulalamika ili hatua stahiki zichukuliwe,” amesema Macho.

Katika hatua nyingine, diwani wa kata ya Majengo, Francis Manyika amesema kumekuwa na changamoto ya walimu kutokaa kwenye vituo vyao vya kazi kutokana na mazingira ya kazi kutokuwa rafiki.

“Walimu wanakimbia kufanya kazi kwenye shule ya msingi ya hapa Mponda kutokana kutokuwa na mazingira rafiki, hakuna nyumba za kuishi walimu, hivyo wanakaa siku mbili wanaondoka, ni vema sasa halmashauri ikaboresha na kutoa motisha kwa watumishi wanaoishi mazingira magumu,” amesema Manyika.