Mbunge ataka BoT izibane benki zishushe riba

Mbunge wa Viti Maalumu (Chadema), Anatropia Theonest akizungumza bungeni alipokuwa akichangia mjadala wa kupitisha makadirio ya mapato na matumizi ya fedha ya ofisi ya Waziri Mkuu na taasisi zake kwa mwaka wa fedha 2021/2022, jijini Dodoma leo. Picha na Edwin Mjwahuzi

Muktasari:

  • Mbunge wa Viti Maalum, Anatropia Theonest ameitaka Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kufanya mabadiliko ya sera zake ili kulazimisha benki nchini kushusha riba za mikopo.

Dodoma. Mbunge wa Viti Maalum, Anatropia Theonest ameitaka Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kufanya mabadiliko ya sera zake ili kulazimisha benki nchini kushusha riba za mikopo.

Anatropia ameeleza hayo leo Jumatano Aprili 14,  2021 wakati akichangia makadirio ya mapato na matumizi ya ofisi ya waziri mkuu mwaka 2021/22.

Amesema kama wakiandaa mazingira mazuri ya wafanyabiashara kwa kufanya kazi katika mazingira wezeshi, sekta binafsi itaweza kuchangia zaidi katika uchumi wa nchi.

Ametaja miongoni mwa changamoto zinazoikuta  sekta binafsi ni mlolongo wa tozo, “usumbufu wa kupata vibali vya kazi lakini ninachotaka kueleza specific ni upatikanaji wa mikopo. Sekta binafsi inawezaje kujiendesha bila kupata mikopo, kuna changamoto ya riba kubwa ya mikopo.”

Amesema taarifa ya BoT ya mwaka 2017 inaonyesha kuwa walifanya maboresho ya riba za benki kwa kushusha  kutoka asilimia 12 hadi asilimia tano lakini akadai wafanyabiashara wanapokwenda katika mabenki kuomba mkopo wanatozwa riba ya zaidi ya asilimia 11.

“..., ni kwa nini tunakuwa na mikopo chechefu? Ni kwa sababu riba zinakuwa juu mtu anakopa fedha biashara ni ngumu anaacha kulipa,” amesema.

Ameomba BoT kufanya maboresho katika sera zake kwa kuhakikisha wanazilazimisha benki kushusha riba.