Mbunge ataka mafunzo ya mgambo yawe sehemu ya mafunzo ya JKT, ajibiwa
Muktasari:
- Mbunge wa Nyasa (CCM), Stella Manyanya ametaka mafunzo ya mgambo kuwa sehemu ya mafunzo ya vijana ya Jeshi la Kujenga Taifa (JKT).
Dodoma. Serikali ya Tanzania imesema hakuna mpango wa kuyafanya mafunzo ya Jeshi la Akiba (mgambo) kuwa sehemu ya mafunzo ya vijana wanaokosa nafasi za kujiunga na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT).
Hayo yamesemwa leo Jumatatu, Aprili 8, 2024 na Waziri wa Ulinzi, Dk Stergomena Tax wakati akijibu swali la msingi la Mbunge wa Nyasa (CCM), Stella Manyanya.
Manyanya amehoji kuna mpango gani wa kufanya mafunzo ya mgambo kuwa sehemu ya mafunzo kwa vijana wanaokosa nafasi ya kujiunga na JKT.
Akijibu swali hilo, Dk Tax amesema Jeshi la Akiba (Mgambo) lilianzishwa kwa Sheria ya Jeshi la Akiba Nambari 2 ya mwaka 1965.
Amesema lengo ni kuandaa nguvu ya akiba kwa ajili ya kusaidia jeshi la kudumu wakati wa vita, operesheni na majanga na kuuandaa umma wa Watanzania, ili waweze kuelewa kuwa dhana ya ulinzi wa Taifa ni jukumu la kila Mtanzania.
Amesema vijana 600 kutoka kila mkoa hupata mafunzo kila mwaka.
Dk Tax amesema JKT lilianzishwa kupitia Sheria ya Jeshi la Kujenga Taifa Sura ya 193 iliyorejewa Mwaka 2002 kwa malengo ya ulinzi wa Taifa, kujenga uzalendo na mshikamano, uzalishaji mali, na kutoa elimu ya kujitegemea.
Amesema kuanzishwa kwa vyombo hivyo kulilenga mahitajio tofauti.
“Kwa muktadha huo, hakuna mpango wa kuyafanya mafunzo ya Jeshi la Akiba kuwa sehemu ya mafunzo ya vijana wanaokosa nafasi za kujiunga na Jeshi la Kujenga Taifa,” amesema.
Amesema vijana wenye sifa wanaruhusiwa kuomba kujiunga na mafunzo ya Jeshi la Akiba.
Katika maswali ya nyongeza, Manyanya amesema Jeshi la Akiba linaonekana kuwa na hadhi tofauti kidogo ukilinganisha JKT.
“Tumeshuhudia hata wakati wa ajira zinalenga zaidi JKT, katika baadhi ya ameneo, je Serikali haioni iko haja sasa ya kuboresha kuboresha mafunzo, ili kuvutia vijana na wengi zaidi waweze kwenda huko.
Na kuwezesha uwiano ukizingatia kwamba JKT haina uwezo kwa sasa halina uwezo wa kuchukua wenye uhitaji wa kuitia huko,”amesema.
Akijibu, Dk Tax amesema ni ushahuri mzuri hasa ukizingatia sasa hivi wanaangalia ni jinsi gani wanavyoweza kuwachukua vijana wote wanaostahili kwenda kujiunga na JKT.
Amesema pamoja na mahitajio ya majeshi hayo ni tofauti, watauangalia ushauri huo kama unaweza kufanyiwa kazi na ni kwa namna gani.