Mbunge ataka urudishwe utaratibu kuingia Zanzibar kwa pasipoti
Muktasari:
Amesema anahitaji hati za kusafiria zirudi ili kuwe na ulindaji wa watu wanaoingia Zanzibar, wakiwamo wa kutoka Tanzania Bara.
Dodoma. Baadhi ya wabunge wametaka kero za Muungano kutatuliwa kwa wakati, mwingine akitaka kurejeshwa utaratibu wa kuingia Zanzibar kwa pasipoti (hati za kusafiria).
Hayo yameibuka wakichangia makadirio ya mapato na matumizi ya Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira kwa mwaka 2024/25. Ofisi hiyo imeomba Bunge kuwaidhinishia Sh62.67 bilioni.
Akichangia makadirio hayo bungeni leo Aprili 23, 2024 mbunge wa Konde, Mohamed Said Issa amesema wakati wa utawala wa hayati Mwalimu Julius Nyerere na hayati Abeid Amani Karume kulikuwa na utaratibu wa kuingia Zanzibar kwa pasipoti.
“Kwa nini waliweka pasipoti visiwa vile vinahitaji kulindwa, mimi sikubaliani na suala la kutovilinda visiwa. Sasa hivi Zanzibar imejaa watu na tunavyoendelea hawatakuwa na sehemu ya kuishi.”
“Sasa hivi ukienda pale Zanzibar utakuta viwanja vimechukuliwa, miti imekatwa, kulikuwa na zao la mikarafuu haliko tena, imebakia Pemba nako linaenda kuisha, minazi hakuna sasa hivi tunaagiza nazi kutoka Mafia,” amesema.
Amesema hata ajira za watalii hawapati tena Wazanzibari bali wageni, hivyo kutaka uwepo wa mikakati ya kulinda Wazanzibari.
Kuhusu kero za Muungano, amesema Serikali inatakiwa kuzimaliza kwa sababu walishaziainisha.
“Kama ni kero ambazo zinaweza kutatulika basi tuzitatue, jambo hili la kusema kero zimebakia hizi zitatuliwa si sahihi. Kwa sababu bajeti iliyopita, mwaka juzi tunasema hivyo, ni lini zitaisha au tuseme kuwa Muungano huu ni wa kero?” amehoji.
Naibu Waziri katika Ofisi ya Makamu wa Rais, Khamis Hamza Khamis, alimpa taarifa kuwa utatuzi wa changamoto hizo una utaratibu wake na si kuwa inapotokea changamoto wanakutana na kutafutia ufumbuzi.
Amesema kuna utaratibu unaotumika katika kutatua changamoto hizo kupitia kamati, tume ambazo zinaunganisha pande zote mbili za Muungano.
“Asifikirie kwamba changamoto zote tutatatua siku moja, aipe Serikali muda itazitatua kwa mujibu wa taratibu,” amesema.
Issa alikataa taarifa hiyo na kusema haina afya na kusisitiza kuwa Wazanzibari wana upenda Muungano na ni mzuri lakini kero zinazojitokeza ndiyo shida.
Mbunge wa Viti Maalumu, Saada Mansour Hussein amesema pamoja mafanikio yaliyopatikana bado kuna changamoto zinazohusiana na watendaji kushindwa kuutafakari kwa vitendo Muungano.
Ametoa mfano wa changamoto ya kusumbuliwa kwa watu wanaotoka na kuingia Zanzibar bandarini, ni kuwa wanashindwa kuvuka na vitu.
“Wengine tuna ndugu zetu (Tanzania Bara), tumeolewa huku tukitoka na zawadi zetu na kufika pale bandarini ni tatizo. Nimeenda kijiji kwa wifi zangu nimepewa zawadi nyingi lakini imenibidi nitumie hapahapa Dodoma kwa sababu siwezi kwenda nazo Zanzibar,” amesema.
Mbunge wa Viti Maalumu, Khadija Hassan Aboud ameshauri Serikali kuendelea na juhudi za haraka na za mara kwa mara za kutatua changamoto za Muungano.
Alitaka utatuzi wa kero za Muungano kufanyika kwa wakati hasa kwa zile zinazohusu maisha, uwekezaji, hali na uchumi wa Mtanzania.
Mbunge wa Pandani, Maryam Omary Said alisema kinachowaumiza wabunge wa majimbo wa Zanzibar ni mfuko wa jimbo kuongozwa na sheria mbili tofauti.
“Pesa ya mfuko wa jimbo inapotoka hapa Bara inakuwa salama na tuko sawa na wenzetu wote bila ubaguzi, lakini inapofika Zanzibar ikaingia katika mfuko wa Makamu wa Rais inakuwa ni changamoto kubwa inayoninyima uhuru kama mbunge,” amesema.
Maryam amesema ni wakati sasa Serikali kupeleka marekebisho ya sheria hiyo bungeni, ili wabunge wapate uhuru na fedha za mfuko wa jimbo.
Utatuzi wa hoja za Muungano
Akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya ofisi yake, Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Makamu wa Rais, Dk Seleman Jafo amesema katika vikao vya kamati za pamoja za kushughulikia masuala ya Muungano, hoja nne zilijadiliwa.
Amezitaja hoja hizo ni mgawanyo wa mapato yatokanayo na hisa za Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) zilizokuwa katika Bodi ya Sarafu ya Afrika Mashariki na faida ya Benki Kuu, mapendekezo ya Tume ya Pamoja ya Fedha, usajili wa vyombo vya moto na uingizaji wa sukari kutoka Zanzibar katika soko la Tanzania Bara.
Dk Jafo amesema wizara zenye hoja zimepewa maagizo ya kuzipatia ufumbuzi hoja hizo.
“Napenda kulihakikishia Bunge, Serikali zote mbili zina nia ya dhati na thabiti kuhakikisha kuwa hoja za Muungano zilizopo na zitakazojitokeza zinashughulikiwa kwa ushirikiano mkubwa, kwa lengo la kuulinda na kuudumisha Muungano wetu adhimu,” amesema.