Mbunge ataka vyama vya siasa vianzishe dawati la jinsia

Neema Lugangira

Muktasari:

  • Mbuge wa Viti Maalumu, Neema Lugangira ameiomba Ofisi ya Waziri Mkuu kusimamia uanzishwaji wa madawati ya jinsia ndani ya vyama vya siasa, kwa kuwa tayari sheria imesainiwa na Rais Samia Suluhu Hassan na nchi inakwenda kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa mwaka huu.

Dodoma. Mbunge ameikata Ofisi ya Waziri Mkuu kuhakikisha vyama vya siasa vinafuatiliwa vitekeleze sheria inayovitaka kuanzisha madawati ya jinsia ndani yake.

Kauli hiyo imetolewa leo Ijumaa Aprili 5, 2024 na Mbunge wa Viti Maalum, Neema Lugangira wakati akichangia mjadala wa makadirio ya bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwamba Rais Samia Suluhu Hassan amesaini miswada ya sheria ya uchaguzi na vyama vya siasa na sasa imekuwa sheria.

Lugangira amesema miongoni mwa vipengele kwenye muswada wa mabadiliko ya sheria ya vyama vya siasa ni vyama hivyo kuanzisha madawati ya jinsia yatakayoshughulikia matatizo ya unyanyasaji wa wanawake wanaojitosa kwenye siasa.

Amesema kwa kuwa miswada hiyo imekuwa sheria, basi Ofisi ya Waziri Mkuu ivifuatilie vyama vya siasa kuhakikisha vinaanzisha madawati hayo.

“Mheshimiwa Spika naiomba Ofisi ya Waziri Mkuu kuvitaka vyama viweke tarehe ya kuanzisha madawati hayo,” amesema.

Amesema mwaka huu Tanzania inakwenda kwenye uchaguzi wa Serikali za mitaa hivyo, kuanzishwa madawati hayo mapema ni jambo la msingi.

Serikali iliwasilisha bungeni muswada wa mabadiliko ya sheria ikiwamo suala la kuanzishwa dawati la jinsia kwenye vyama vya siasa baada ya kuwepo malalamiko ya wanawake kudhalilishwa ikiwamo udhalilishaji wa kingono na hasa wakati wa uchaguzi kuanzia ndani ya vyama.