Mbunge CCM ahoji walimu kusimamia ujenzi wa shule

Mbunge wa Viti Maalumu, Munde Tambwe akizungumza bungeni alipokuwa akichangia mjadala wa kupitisha Bajeti Kuu ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2022/2023, jijini Dodoma leo.  Picha na Edwin Mjwahuzi

Muktasari:

  • Mbunge wa viti maalum (CCM), Munde Tambwe ameitaka Serikali kuachana na utaratibu wa walimu wakuu kupewa kazi ya kusimamia ujenzi katika shule zao kwa kuwa si wataalamu wa mambo ya ujenzi na uhasibu.



Dodoma. Mbunge wa viti maalum (CCM), Munde Tambwe ameitaka Serikali kuachana na utaratibu wa walimu wakuu kupewa kazi ya kusimamia ujenzi katika shule zao kwa kuwa si wataalamu wa mambo ya ujenzi na uhasibu.

Munde ameyasema hayo leo Alhamisi Juni 16, 2022  wakati akichangia mjadala wa bajeti kuu ya Serikali kwa mwaka 2022/23.

“Tumekuwa tukifanya mambo ya ajabu, fedha zinakwenda kwenye shule  kujenga madarasa na kadhalika, anaambiwa mwalimu mkuu asimamie majengo. Mwalimu mkuu ana utaalamu gani wa kusimamia majengo," amehoji.

Amesema walimu hao hawajasomea uhasibu lakini wanakwenda kukaguliwa na kwamba  shule ina walimu wachache lakini anatolewa mwalimu mkuu kwenda kusimamia ujenzi wakati wamekuwa wakilalamikia kuwa idadi yao haitoshi nchini.

“Niiombe Serikali itafute wataalam wa kufanya hiyo kazi na walimu waachwe wafanye kazi zao za elimu. Wamekuwa wakilaumiwa sana katika hili. Kwa mfano jengo la nyumba ya mwalimu linajengwa kilometa moja kutoka shuleni nani anampa hiyo nauli ya kwenda kusimamia jengo hilo,” amesema.

Aliitaka Serikali kutowakamata walimu hao inapotokea kasoro katika ujenzi kwa sababu si wahandisi wa kuweza kusimamia ujenzi wa majengo hayo.