Mbunge Mafuwe aitaka jamii kutowaficha wenye ulemavu
Mbunge wa Hai, Saashisha Mafuwe akiwa anamwendesha mtoto mwenye ulemavu baada ya kukabidhi msaada wa viti mwendo vitano kwa wazazi wa watoto hao. Picha na Janeth Joseph
Muktasari:
Mbunge wa Hai, Saashisha Mafuwe amewataka wazazi wenye watoto wenye ulemavu wilayani humo kutowaficha ndani badala yake wawapeleke shule kwani wana haki ya kupata elimu kama watoto wengine.
Hai. Mbunge wa Hai, Saashisha Mafuwe amewataka wazazi wenye watoto wenye ulemavu wilayani humo kutowaficha ndani badala yake wawapeleke shule kwani wana haki ya kupata elimu kama watoto wengine.
Mafuwe ameyasema hayo leo Jumapili Januari 16, 2022 wakati akiwakabidhi viti mwendo vitano (wheel chairs) watoto wenye ulemavu wilayani humo ambapo amesema ametoa viti mwendo hivyo ili wazazi wasiendelee kuwaficha watoto ndani.
"Lengo la kuleta hivi viti mwendo ni kuwafanya hawa watoto wasikae tu ndani, hawa ni watoto kama watoto wengine, wana haki ya kupata elimu kama walivyo watoto wengine pamoja na kupendwa, niwaombe wazazi wenye watoto kama hawa wasiwafiche ndani, tuwasaidie na tuwapende,"amesema Mafuwe
Aidha amewataka wale wote ambao wamepewa dhamana na Serikali ya kuwasaidia watoto hao watumie nafasi zao kuwasaidia huku akiitaka jamii kuendelea kuibua watoto wenye ulemavu waliofichwa na wazazi wao.
Naye ofisa elimu maalumu wa Wilaya hiyo, Hidaya Kirima amesema mpaka sasa wameweza kuwabaini watoto 100 wenye ulemavu ambao walikuwa hawajulikani kwenye jamii ambapo amesema tayari wilaya hiyo ina shule 38 ambazo zinatoa elimu jumuishi.
"Moyo wangu umepata faraja ya tofauti kabisa, nilipokuja Hai nilitembelea kata zote 17 ambapo tuliweza kuwabaini watoto zaidi ya 100 wenye mahitaji maalumu, mwaka jana tulikuwa na wanafunzi 29 waliofanya mtihani wa darasa la saba katika shule zetu na 27 wamefanya vizuri katika masomo yao,"amesema Hidaya
Mmoja wa wazazi wa watoto hao, Fatuma Abdallah amemshukuru mbunge wa Hai kwa kutoa msaada wa viti hivyo ambapo amesema itamsaidia sasa kwenda kufanya majukumu yake ya kujitafutia riziki kwani alikuwa hawezi kutoka nyumbani kutokana na changamoto ya mwanaye.
"Nilikuwa siwezi kufanya chochote wala kutoka nyumbani, namshukuru mbunge kwa kutusaidia sasa hivi nitaweza kutoka angalau kwenda kutafuta riziki ya maisha,maana nitaweza kumweka mtoto kwenye kiti na kufanya shughuli zangu bila shida yoyote,"amesema Fatuma