Mbunge: Simba wavamizi wasakwe, waingia Kilolo

Mbunge wa Jimbo la Kilolo wilayani Iringa, Justin Nyamoga amesema anaiomba Serikali kufanya jitihada za kuwasaka simba wavamizi  ambao bado wanaendelea kuvamia na kuua mifugo katika vijiji mbalimbali.

Muktasari:

Mbunge wa Jimbo la Kilolo mkoani Iringa, Justin Nyamoga ameiomba Serikali kufanya jitihada za kuwasaka simba wavamizi ambao bado wanaendelea kuua mifugo katika vijiji mbalimbali katika wialaya za Iringa na Kilolo.

Iringa. Mbunge wa Jimbo la Kilolo mkoani Iringa, Justin Nyamoga ameiomba Serikali kufanya jitihada za kuwasaka simba wavamizi ambao bado wanaendelea kuua mifugo katika vijiji mbalimbali katika wialaya za Iringa na Kilolo.

Nyamoga amesema vijiji vilivyoathirika katika Wilaya ya Kilolo mpaka sasa ni kijiji cha Imalutwa, Kising’a, Lugalo na Ihimbo ambapo jumla ya ng’ombe waliouawa mpaka sasa katika vijiji hivyo ni watatu.

Akizungumza na Mwananchi Digital Leo Juni 29, Nyomoga amesema wananchi wanazidi kutoa taarifa kwamba wamewaona simba huku na kule na taarifa hizi zinaweza kuwa sahihi au sio sahihi hivyo tunaomba serikali wafanye juhudi na wathibitishe kuwa simba wapo maeneo gani katika Wilaya ya Kilolo na kuwakamata kuwarudisha hifadhini.

Nyamoga amefafanua kwamba hata hivyo wakazi wa vijiji hivyo wametahadharishwa kutembea usiku na na hata mchana wanapotembea, basi wawe katika makundi kama sehemu ya kujihamina wanyama hao wakali.

"Tunachoomba kwa Serikali ni kutumia njia mbalimbali mbadala ili waweze kuwapata simba hao kwani wananchi mpaka sasa hawana amani kabisa," amesema Nyamoga.

Kamanda wa Hifadhi ya Taifa Ruaha Godwell Ole Meing'ataki amesema bado zoezi la kuwatafuta simba hao linaendelea huku akisema lengo ni kuondokana na madhara yanayoletwa na wanyama hao.

Ole Meing'ataki ameeleza kwamba simba hao wanafanya uvamizi na kuhama kijiji kimoja mpaka kingine hivyo kuwakamata kwa urahisi imekuwa ngumu.

Hata hivyo Ole Meing'ataki ameongezea kwa kusema kuna jitihada ambazo bado zinaendelea kufanyika kwa nguvu zaidi ili simba hao wapatikane kama yalivyo matarajio ya wananchi.

Jumla ya mifugo iliyouawa wilayani Iringa ni ng'ombe 34, Kondoo 4, Mbuzi 7, Nguruwe 7 na kuku mmoja.

"Tuliweka mtego wa ndama na tumeona ndama yule karudi, Askari wa Wanyamapori walichelewa kumdhibiti akakimbia," amesema Ole Meing'ataki.


Naye Diwani wa Kata ya Lugalo Wilaya ya Kilolo Mkoani Iringa Sadaki Msigwa amesema ni kweli matukio ya simba kuvamia baadhi ya vijiji katika Wilaya hiyo bado yanaendelea huku baadhi ya wavijiji wakipoteza mifugo yao.

Msigwa amesema katikati ya vijiji hivyo vilivyovamiwa kuna msitu mkubwa ambao unatenganisha kijiji cha kising'a na Imalutwa na kwamba huenda simba hao wapo katika msitu huo.

Kwa upande wao wananchi wa Kata ya Lugalo wilayani ya Kilolo wamesema simba hao wanahama hama kutoka kijiji kimoja mpaka kingine hivyo hofu bado kubwa kwani hawajui ni wakati gani simba hao watafika maeneo yao.