Mbunge Uganda awasilisha hoja kutambua mchango wa Magufuli

Muktasari:

  • Mbunge wa Bunge la Afrika Mashariki (Eala) kutoka Uganda, George Odongo amewasilisha hoja maalumu ya kutambua mchango wa Rais wa awamu ya tano wa Tanzania Hayati John Magufuli aliyefariki dunia Machi 17,2021.

Arusha. Mbunge wa Bunge la Afrika Mashariki (Eala) kutoka Uganda, George Odongo amewasilisha hoja maalumu ya kutambua mchango wa Rais wa awamu ya tano wa Tanzania Hayati John Magufuli aliyefariki dunia Machi 17,2021.

Katika kikao kilichofanyika kwa njia ya mtandao jana Machi 31, 2021 na kuongozwa na Spika Martin Ngoga, mbunge huyo amesema taarifa za kifo cha Magufuli walizipokea kwa mshtuko mkubwa .

“Kifo chake kilituma ujumbe mzito kwa wananchi wa Tanzania, kanda yote ya Afrika Mashariki na ulimwengu mzima kwa sababu Magufuli alikuwa mwanasiasa mwenye uwezo mzuri baada ya kupata uzoefu katika nafasi za chini kabla ya kuwa Rais,”amesema Odongo.

Amesema wakati wa uhai wake alijitoa kwa ajili ya nchi yake na kuhakikisha Watanzania wanakuwa na maisha bora kwa kuongoza ujenzi wa miundombinu ya barabara, viwanja vya ndege, bandari na maeneo mengine.

“Kipindi cha miaka mitano ya uongozi wake alipata mafanikio makubwa yaliyomtambulisha duniani kote ikiwemo udhibiti wa mapato ya umma yaliyosababisha miradi yote ya Serikali kuwa na thamani ya fedha zilizotumika,” amesema Odongo

Mbunge wa Bunge hilo kutoka Tanzania, Adam Kimbisa amesema kifo cha kiongozi huyo kimeacha majonzi huku akieleza jinsi Serikali chini ya Magufuli ilivyofanya mengi akibainisha kuwa sasa malengo yote yatamalizwa na Rais Samia Suluhu Hassan.