Mbunge wa Mbarali afariki kwa ajali ya pikipiki

Mbunge wa Jimbo la Mbarali (CCM) Francis Leonard Mtega aliyesimama enzi za uhai wake.

Mbeya. Mbunge wa Jimbo Mbarali mkoani Mbeya Francis Mtega amefariki dunia kwa ajali baada ya pikipiki aliyokuwa akisafiria kutoka shambani kurejea nyumbani kugongana na ‘Powertilla’ katika Tarafa ya Ilongo Kata ya Chimala.

Akizungumza na Mwananchi leo Julai Mosi, Mkuu wa Wilaya (DC) ya Mbarali, Kanali mstaafu Denis Mwila amethibitisha kutokea kwa ajali hiyo leo Julai Mosi 2023 saa 9 alasiri baada ya pikipiki aina ya Boxer yenye namba za usajili MC 573 CGY aliyokuwa akiendesha marehemu kugangana na ‘Powertilla.’

Amesema ajali hiyo imetokea kwenye barabara ya vumbi wakati marehemu akitokea shambani kwake akielekea Kata ya Chimala wilayani Mbarali ambako alikuwa akiishi.

“Tayari dereva wa ‘Powertilla’ Alex Musa (18) anashikiliwa na Polisi na chanzo cha ajali ni uzembe wa dereva huyo ambaye hakuchukua tahadhari na kuendelea mwendo mbaya kwenye barabara ya vumbi jambo ambalo lilisababisha ajali hiyo,” amesema Kanali Mwila na kuongeza;

“Tulishatoa tahadhari na masharti madereva wote wa ‘Powertilla’ ifikapo saa 12 jioni kutofanya kazi kutokana na madereva wake kutokuwa na leseni, lakini pia nyingi hazina taa zinazoweza kuonyesha usalama wawapo barabarani,” amesema.

Awali, wakati akitangaza kifo hicho, Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson ametoa pole kwa familia ya marehemu, ndugu, jamaa, wabunge na wananchi wa Jimbo la Mbarali.

“Nimepokea kwa masikitiko makubwa taarifa za kifo cha Mheshimiwa Francis Leonard Mtega. Natoa pole kwa familia ya Marehemu, ndugu, jamaa, Waheshimiwa Wabunge na Wananchi wa Jimbo la Mbarali. Mwenyezi Mungu awape moyo wa uvumilivu na subira katika kipindi hiki kigumu,” amesema Spika Tulia.

Taarifa kutoka Kitengo cha Mawasiliano na Uhusiano wa Kimataifa cha Bunge imesema kuwa Ofisi ya Bunge kwa kushirikiana na familia ya Marehemu inaratibu mipango ya maziko na taarifa zaidi zitaendelea kutolewa.

Kwa upande wa Mwenyekiti wa Wabunge Mkoa wa Mbeya, Oran Njeza amesema kuwa amepokea taarifa za kifo cha Mbunge huyo na kwa sasa yuko njiani kurejea Mbeya akitokea Dodoma.

“Ni kweli nimepokea taarifa za kifo chake bado tunaendelea kufuatilia kwani kwa sasa nipo njiani natokea Dodoma kurejea Mbeya,” amesema.

Naye Mbunge wa Lupa Wilaya ya Chunya, Masache Kasaka amesema wamepokea taarifa za kifo hicho kwa mshtuko mkubwa kwani hivi karibuni walikuwa naye kwenye vikao vya Bunge mjini Dodoma.

“Tumempoteza mtu muhimu sana alikuwa na ushirikiano mkubwa na wabunge wenzake na kwamba wamepokea taarifa hizo kwa mshtuko mkubwa sana,” amesema.

Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake (UWT) Wilaya ya Mbarali, Zabibu Nuroo amesema kama chama wamepokea taarifa hizo kwa mshtuko mkubwa na kwamba wamepoteza mtu muhimu aliyekuwa akiwaunga mkono kwa hali na mali

“Kimsingi binafsi nimepata pigo kubwa sana kutokana na juhudi zake kuunga mkono shughuli za chama kwa sasa tunasubiri taratibu za kifamilia ili kujua maziko taratibu za maziko,” amesema.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Benjamin Kuzaga amesema kwa sasa yuko njiani anaelekea Wilaya ya Mbarali na atatoa taarifa kamili mara baada ya kufika eneo la tukio.